Trafiki Alierekodiwa Akipewa Rushwa Ashughulikiwa

Trafiki Alierekodiwa Akipewa Rushwa Atimuliwa
ASKARI wa Kikosi cha Usalama Barabarani, ambaye video yake ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii jana ikimwonyesha akipokea rushwa ya Sh. 5,000, amefukuzwa kazi kwa fedheha na Jeshi la Polisi.


Video hiyo ambayo ilianza kusambaa kwenye makundi mbalimbali ya kijamii ya WhatsApp na Facebook jana mchana, inamwonyesha askari huyo akipokea kiasi hicho cha fedha iliyoambatanishwa na leseni eneo la Mwenge, jijini Dar es Salaam, pengine mapema wiki hii.

Katika tukio hilo, dereva mmoja aliyeombwa rushwa alimrekodi askari huyo kupitia simu yake ya mkononi wakati akimpatia rushwa hiyo iliyowekwa chini ya leseni.

Dereva huyo akiwa ametegesha kamera yake kwenye gari, askari huyo alifika kwenye kioo cha mlango wa dereva na kumrudishia leseni yake ambayo alikuwa nayo tayari, kisha askari huyo kumwomba ampatie leseni hiyo kwa mara nyingine ikiwa na rushwa.

Baada ya dereva kurudishiwa leseni, aliiunganisha na Sh. 5,000 aliyoiweka kwa chini na kumrudishia askari ambaye naye alikuwa akijifanya kama anatoa risiti kwenye mashine yake kielektroniki aliyokuwa ameishika mkononi.

Baada ya kupokea leseni iliyokuwa ikiwa imeambatanishwa na fedha hizo, trafiki huyo alichukua fedha na kumrudishia leseni dereva huyo kisha kuondoka.

Akizungumza na Nipashe jana jijini Dar es Salaam,  Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi wa Polisi Jumanne Murilo, alisema tayari askari huyo ameshachukuliwa hatua kwa kufukuzwa kazi tangu Jumanne.

Kamanda Murilo alisema askari huyo hadi anafukuzwa kazi ndani ya Jeshi la Polisi alikuwa amefanya kazi kwa muda wa mwaka mmoja na nusu.

"Tukio hili lilifanyika eneo la Mwenge na baada ya kulibaini tulianza uchunguzi wetu ambao juzi (Jumanne) ulikamilika na kubaini tukio hilo lilikuwa la kweli (kwamba) amepokea rushwa. Hivyo tumemuondoa kazini," alisema.

Kamanda Murilo ambaye hakumtaja jina askari huyo aliwakumbusha trafiki kuzingatia maadili ya kazi na taratibu za kijeshi zilizowekwa.

Vitendo vya kuwachukua video trafiki wanaopokea rushwa vimekuwa vikijitokeza mara kwa mara ambapo tukio lingine linalofanana na hilo lilitokea mkoani Tanga mwaka 2015.

Katika tukio hilo, aliyekuwa askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Koplo Anthon Temu, mwenye namba F785 alifukuzwa kazi kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa.

Tukio hilo lilithibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Zuberi Mwombeji ambaye alisema lilitokea barabara kuu ya Chalinze-Segera.

Alisema kupitia mitandao ya kijamii, askari huyo alionekana akipokea rushwa kutoka kwa dereva wa gari alilokuwa amelisimamisha kwa ajili ya kukagua makosa yanayoweza kuhatarisha usalama barabarani.

Tukio lingine ni lile lililotokea visiwani Zanzibar mwaka uliopita, baada ya Sajini Hamad Kassim wa Kituo cha Mkokotoni visiwani humo, kuonekana kwenye video akipokea rushwa ya Sh. 10,000.

Rushwa hiyo aliiomba kutoka kwa raia wa kigeni baada ya kumkamata akiwa hajafunga mkanda wakati akiendesha gari.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad