Trump Ataka Kuonyesha Nguvu Zake za Kijeshi

Trump Ataka Kuonyesha  Nguvu Zake za Kijeshi
Rais wa Marekani Donald Trump anaripotiwa kuwauliza maafisa wakuu wa jeshi kuandaa gwaride kubwa zaidi nchini humo kuonyesha nguvu zake za kijeshi.

Afisa anayehusika na masuala ya habari katika ikulu ya white house, Sarah Sanders amesema rais Trump amewaagiza wakuu wa jeshi kupanga hafla hiyo ambayo raia wa taifa hilo watatoa shukrani na heshima zao kwa wanajeshi wao.

Ripoti zinasema kuwa rais Trump alifurahishwa mno na sherehe za Bastille nchini Ufaransa, ambako mbali na wanajeshi kuonyesha wanajeshi wake, magari ya kivita na vifaru pia inajumuisha maonyesho ya ndege za wana anga.

Siku ya kuwakumbuka wakongwe wa kivita huadhimishwa tarehe kumi na moja Novemba kila mwaka na inasemekana huenda sherehe hizo zikaandaliwa siku hiyo.

Tayari maeneo matatu ambayo huenda yakafikiriwa kuandaa sherehe hizo yametolewa.

Rais Trump anasemekana kupendekeza sherehe hizo kuandaliwa katika barabara ya Pennsylvania inayoliunganisha bunge la congress na ikulu ya white house na hoteli ya Trump International.

Lakini kuna wasi wasi kuwa baada ya sherehe hizo bara bara hiyo huenda ikaharibiwa kabisa kutokana na uzito wa vifaa vya kijeshi.

Tamasha za kijeshi sio za kawaida nchini Marekani kwa sababu ni ghali.

Sherehe za mwisho za kijeshi kuandaliwa baada ya vita vya ghuba iligharimu serikali dola milioni kumi.

Wanasiasa wa chama cha Democratic wameshutumu mpango huo kwa gharama kubwa na kusema kuwa fikra hizo zinatoa ishara za kutia wasiwasi.

"Ni njia ovyo ya kupoteza fedha!" alituma ujumbe wa twitter mwakilishi Jim McGovern. "Trump anaonekana kuwa dikteta zaidi ya rais , Wamarekani wanastahili kiongozi bora zaidi."

Mwakilishi Jackie Speier, ambaye ni mwanachama wa kamati ya bunge kuhusu huduma za kijeshi ameliambia shirika la utangazaji CNN: "Nilishangazwa na pendekezo hilo kwa kweli .... tuna kiongozi anayetaka kuwa kama Napoleon."


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad