Uchambuzi wa Shaffih Dauda kuelekea Simba vs Azam leo Februari 7, 2018

Simba na Azam zinakutana kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania bara, hii ni mara ya pili timu hizi kukutana msimu huu huku kila timu ikiwa na nafasi ya kushinda taji la ligi msimu huu (2017/18) endapo kila timu itaendelea kufanya vizuri kwenye michezo yake iliyosalia wakati huu wa mzunguko wa pili.

Watoto wa Msimbazi ndio vinara wa ligi wakiwa wanaongoza kwa pointi zao 38 baada ya mechi 16 wakifuatiwa na watani zao Yanga ambao wana pointi 34 katika nafasi ya pili lakini wakiwa wamecheza mechi 17, Azam inasimama nafasi ya tatu ikiwa na pointi 33 kabla ya mchezo wa leo wakati Singida United ikiwa nafasi ya nne kwa pointi zao 30 kati ya miamba inayowania ubingwa.



Katika mchezo huu (Simba vs Azam) ili kila timu iendelee na dhamira yake ya kuchukua ubingwa inatakiwa ipate matokeo ya ushindi dhidi ya timu ambayo ni adui yake kwenye mbio za ubingwa, kwa hiyo ni mechi nzuri sana ambayo itakuwa na mvuto wa kipekee.

Bocco vs Azam mara ya pili



John Bocco amekuwa kwenye kiwango bora siku za karibuni, anakutana na Azam timu ambayo ana historia nayo, hadi sasa Bocco ameshafunga magoli tisa kwenye ligi huku akiwa amefunga magoli manne mfululizo katika mechi mbili zilizopita (Simba vs Singida United na Simba vs Ruvu Shooting).

Nahodha huyo wa zamani Azam atakuwa akiungana na Aishi Manula, Erasto Nyoni na Shomari Kapombe ambaye huenda akacheza kwa mara ya kwanza dhidi ya Azam tangu alipondoka na kurejea Simba, nyota hao wanne waliondoka kwa pamoja Azam na kusajiliwa Simba, mchezo wa awali uliochezwa Azam Complex, Kapombe peke yake ndio hakucheza kati ya waliondoka Azam kujiunga na Simba.

Simba ya sasa si ya Omog

Wakati Azam ilipokuwa mwenyeji wa mchezo wake wa kwanza msimu huu dhidi ya Simba, Joseph Omog alikuwa bado kocha mkuu wa Simba akisaidiwa na Jackson Mayanja ambaye baadae alijiuzulu, mchezo huo ulimalizika kwa suluhu lakini Simba ya sasa ipo chini ya makocha wapya na imekuwa tishio siku za karibuni.



Simba imebadilika ukiangalia walivyocheza mechi za hivi karibuni, usajili wa Asante Kwasi umeimarisha safu ya ulinzi, wamefunga magoli mengi na kuzuia kuruhusu magoli mengi. Simba imefunga magoli 38 huku ikiruhusu magoli sita (6) ya kufungwa katika mechi 16 ilizocheza hadi sasa, ndiyo timu pekee iliyofunga magoli mengi na kufungwa machache, hiyo inaonesha makali ya washambuliaji na viungo lakini pia ubora wa safu ya ulinzi.

Uwepo wa Said Ndemla na Jonas Mkude kwenye kikosi cha kwanza cha Simba imekuwa tofauti na msimu ulivyoanza, unaona faida  ya mchezaji kukaa benchi kwa sababu imewaletea ukomavu kwa sababu zamani mchezaji akikaa benchi akirudi anakuwa amekwisha lakini baada ya Mkude na Ndemla kupata nafasi wameonesha wanataka kuendelea kucheza kwenye kikosi cha kwanza kutokana na namna wanavyojituma.



Chini ya Omog wawili hao hawakuwa na nafasi za kudumu kwenye kikosi cha kwanza lakini baada ya timu kuwa chini ya Masoud Djuma na baadae ujio wa kocha mpya Pierre Lichantre umewafanya wawe wapya huku viwango vyao vikimshawishi kila mtu kuamini uwezo na ubora wa vijana hao waliolelewa katika klabu hiyo.

Azam si ya kubeza

Ukiitazama Azam lazima uwataje Razaq Abarola, Himid Mao, Mohamed Yakubu na Agrey Morris ambao wamekuwa katika viwango vya juu katika kikosi chao tangu kuanza kwa msimu huu huku wakicheza michezo mingi ya ligi ukilinganisha na wachezaji wengine ambao wamekuwa wakipishana kwenye kikosi.



Kinachowabeba Azam hadi sasa ni safu yao ya ulinzi, Yakubu, Razaq, Agrey Morris, wamecheza kwa viwango vya juu hadi sasa  wakiwa wameruhusu magoli saba kwenye wavu zao lakini pia sehemu ya kiungo Salmin Hoza ameleta changamoto mpya katika idara hiyo.



Azam haifungi magoli ya kutosha

Eneo ambalo linaonekana lina mapungufu kwa Azam ni idara ya ushambuliaji. Mbaraka Yufuph mara nyingi amekuwa akisumbuliwa na majeraha lakini Yahaya Zayd, Shabani Chilunda, Peter Paul kijana ambaye kila akipata nafasi anataka kumfurahisha kocha na kuonesha anastahili kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza, vijana hao wakikomaa wataisaidia Azam kufikia malengo.

Azam imefunga magoli 19 tu katika mechi 16 ilizocheza hadi sasa wakati John Bocco na Emanuel Okwi kwa pamoja wameifungia Simba magoli 19 (Okwi 12, Bocco 9).



Azam wana kumbukumbu nzuri dhidi ya Simba, waliifunga 1-0 kwenye mchezo wa Mapinduzi Cup hatua ya makundi Januari 6, 2018 kwenye uwanja wa amaan visiwani Zanzibar huo ndiyo mchezo wa mwisho kuzikutanisha timu hizo siku za hivi karibuni
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad