Ujumbe wa Mwisho wa Marehemu Akwillina Unasikitisha

Mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) aliyepigwa risasi Februari 16, 2018 eneo la Mkwajuni-Kinondoni jijini Dar na kufariki dunia, kabla ya tukio hilo alitoa ujumbe wa kusikitisha kwa familia yake kabla ya kupatwa na mkasa huo, Uwazi limeelezwa.

 Mwanafunzi huyo aliyekuwa anasoma Shahada ya Kwanza ya Ununuzi na Ugavi (Procurement and Logistics), Akwillina Akwilini alizungumza na mmoja wa ndugu zake wakati akiwa hajui nini kitampata saa chache zijazo, kwa mujibu wa ndugu yake, Ester Michael.

Ndugu yake huyo alisema, Akwillina alimwachia ujumbe mzito ambao unazunguka kichwani mwake na kila alipomsimulia mwanafamilia yeyote aliishia kutokwa na machozi.


Aliniambia: “Mimi ninasafiri (alikuwa akienda Bagamoyo), lakini sijajua nitarudi lini. Unajua ninapambana na maisha, nataka nitoke, lakini pia nataka niwasaidie wazazi wangu (wazazi wake ni wakulima na wafugaji), kwa hiyo niombee tu kwani na wewe pia utanufaika na mafanikio yangu.”

 Akaongeza kuwa, licha ya ujumbe huo, alimwambia kwamba wakati anakazana na elimu, yeye msanii akazane na sanaa yake ili waweze kusaidiana kuinua familia yao.

Baadhi ya marafiki wa marehemu akiwemo Jack John alisema polisi wanatakiwa kuwa makini na silaha za umma kwa sababu zinasababisha vifo kwa watu wasio na hatia.

“Unakumbuka tukio la Iringa ambalo mwanahabari Mwangosi aliuawa kwa bomu? Kuanzia pale walitakiwa kuwa makini na tahadhari na silaha wanazokabidhiwa,” alisema Jack huku akitokwa na machozi.

NDUGU WATAKA HAKI ITENDEKE

Tugolena Richard Uiso, ambaye ni dada wa Akwillina aliyekuwa akiishi naye maeneo ya Mbezi-Luis jijini Dar, akizungumza na gazeti hili alisema kuwa, familia ilishtushwa na taarifa za kifo chake na akaiomba serikali itende haki kutokana na kifo cha ndugu yake.

Alisema awali hawakuamini kuwa mdogo wake alikuwa amefariki dunia kwa sababu walijua yupo chuoni.

“Ijumaa iliyopita tulipata taarifa kuwa amepigwa risasi Kinondoni na amepelekwa hospitalini Mwananyamala, tulishangaa kwa sababu ndugu yangu hakuwa na jambo la kusababisha apigwe risasi, ikabidi twende kuhakikisha ile taarifa,” alisema na baada ya kwenda hospitalini waliutambua mwili na kuthibitisha kuwa ndiye mtoto wao.


HAKUWA KWENYE HARAKATI ZA SIASA

“Wenzetu walipokwenda Polisi Oysterbay, waliambiwa mwili utapelekwa Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi, lakini sisi tunataka haki itendeke katika hili kwa sababu mdogo wangu hakuwa kwenye harakati za kisiasa, alikuwa akifuatilia mambo yake ya masomo, tumebaki na simanzi, tunasubiri kinachoendelea,” alisema.

Alisema Akwillina ni mtoto wa sita kwa wazazi wake wanaoishi Olele wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro na akafafanua kuwa wazazi wake hao wanajishughulisha na kilimo na ufugaji na marehemu alifika Dar kwa ajili ya masomo.

MITANDAONI

Kutokana na tukio hilo, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu katika taarifa kwa vyombo vya habari ulisema ulipokea kwa masikitiko kifo cha mwanafunzi huyo.

“Mauaji haya ya kikatili yanasikitisha sana na sisi kama watetezi wa haki za binadamu tunalaani vikali vitendo hivyo kwa kuwa ni kinyume kabisa na haki za binadamu,” ilisema taarifa hiyo iliyosainiwa na mratibu wake, Onesmo Olengurumwa.

“Tunaviomba vyombo husika kuchukua hatua stahiki kwa waliotekeleza mauaji ya raia wasiokuwa na hatia,” ilisema taarifa hiyo.







RAFIKI YAKE ANENA

Rafiki wa mwanafunzi huyo, Hidaya Shaaban alisema kuwa, siku hiyo ya tukio Akwillina alimuaga kuwa anaelekea Bagamoyo mkoani Pwani kupeleka barua ya mafunzo kwa vitendo.

“Najisikia vibaya na nimeumia, aliniaga anakwenda kupeleka barua yake ya ‘field’ na alikuwa nayo kweli, jioni nikashangaa kupata taarifa kuwa amepata ajali na sikujua ajali gani, lakini baadaye nikaambiwa mauti yamemfika,” alisema.

Alisema awali hakujua kama alifariki dunia kwa kupigwa risasi.

Gazeti hili lilishuhudia watu wengi waliofika nyumbani kwa dada wa marehemu, Mbezi-Luis, eneo la Kaburi Moja wakiwa na majonzi na wengine kuzimia baada ya kulia mno wakati maombolezo yakiendelea.

 WANASIASA

Chama cha ACT Wazalendo kilisema kuwa, kilipokea kwa masikitiko tukio la mauaji ya mwanafunzi huyo.

“Tunasikitika na tunakataa kuona Tanzania inaingia katika ubaguzi wa vyama. Utu na heshima ya binadamu wa Tanzania hauwezi kupimwa na uvyama, tunaomba viongozi wa dini na makundi mengine ya kijamii kukemea mauaji haya,” ilisema taarifa hiyo iliyotolewa na mwenyekiti wake, Yeremia Maganja.

Februari 17, 2018, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa alikiri mtu mmoja kupigwa risasi na polisi wakati wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakiandamana.

 ILIVYOKUWA SIKU YA TUKIO

Wafuasi hao wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe waliandamana kuelelea ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kinondoni, Aron Kagurumjuli kudai viapo vya mawakala wa chama hicho.

Ofisa Uhusiano wa NIT, Ngasekela David alisema kuwa wamepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha wanafunzi huyo.

 “Tumepokea kwa masikitiko taarifa hizi. Tunaendelea kufuatilia zaidi,” alisema David.

Hata hivyo, licha ya kusema kwamba wamepata taarifa za tukio, David alisema kuwa, suala hilo lipo katika mikono ya polisi na familia yake.

“Tulipata taarifa za msiba wa mwanafunzi huyu kutoka kwa mwanafunzi mwenzake aliyekuwa akiishi naye kwenye chumba kimoja nje ya chuo, tumesikitishwa na kifo chake hivyo tunaendelea kuwasiliana na familia kujua utaratibu,” alisema.



Baada ya taarifa za kifo cha mwanafunzi huyo kufika NIT, vilio, huzuni na majonzi vilitawala. Hata juzi mchana wakati waandishi wetu walipofika chuoni hapo, waliwakuta wanafunzi wakiwa katika vikundi huku karibu wote wakiwa na nyuso za huzuni.

Paul Sabuni ambaye ni kiongozi wa darasa alilokuwa akisoma marehemu, alisema kabla ya kifo chake alifika chuoni kusaini ‘course work’.



“Alikuja saa tisa kuangalia matokeo yake na kwa kweli alikuwa amefanya vizuri, alikuwa msichana mzuri anayejituma darasani, tumeumia mno. Sikuwahi kusikia kama anajihusisha kwa namna yoyote na siasa wala chama,” alisema Sabuni ambaye ni Waziri wa Mikopo wa Serikali ya Wanafunzi wa NIT.

Imeandikwa na Richard Bukos na Mayasa Mariwata.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad