SIKU tatu zikiwa zimepita tangu kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Maftah (22), imeelezwa alipanda daladala ambalo mauti yalimfika humo akipeleka barua ya kuomba kufanya mazoezi kwa vitendo aliyokuwa akitarajia kuanza Jumatatu ijayo mkoani Pwani.
Akwilina alipigwa risasi akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni na polisi waliokuwa wakijaribu kutawanya maandamano ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ijumaa jioni.
Rais John Magufuli jana alisema katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii ya Twitter kuwa "Nimeviagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha tukio hili."
Rais Magufuli pia alielezea kusikitishwa "sana" na kifo cha Akwilina, na kutoa pole kwa familia, ndugu, wanafunzi wa NIT na wote walioguswa na msiba huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako alisema marehemu alikuwa ni miongoni mwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.
Aidha, Prof. Ndalichako alisema siku ya Ijumaa Akwilina alikuwa njiani kupeleka barua ya kuomba kufanya kazi kwa vitendo katika moja ya kampuni zilizopo Bagamoyo mkoa wa Pwani.
Marehemu alipanda daladala linalofanya safari kati ya Mabibo na Makumbusho katika kituo cha NIT na kufuatia maelezo ya waziri kwamba alikuwa akielekea Bagamoyo, ilikuwa ashuke mwisho wa safari kabla ya kuunganisha daladala nyingine kwenda Bunju Sokoni au Tegeta Nyuki zilizo stendi za Bagamoyo.
Taarifa za kipolisi zilizotolewa jana zilisema mwili wa marehemu aliyekuwa amekaa kiti cha nyuma katika daladala hiyo yenye namba T558 CSX aina ya Nissan Civilian, ulikutwa ukiwa na jeraha kubwa kichwani lililooneka kutokana na kupigwa na kitu chenye ncha kali, kilichoingia upande wa kulia na kutoka upande wa kushoto.
Prof. Ndalichako alisema Akwilina alikuwa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Ununuzi na Ugavi katika chuo hicho.
"Wizara yangu itagharamia mazishi yake hadi hapo atakapopumzishwa katika makao yake ya milele," alisema Prof. Ndalichako. "Tutasimamia shughuli zote za msiba huo.
"Tunatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki... kwa uongozi wa NIT, kwa wanafunzi na wananchi wote.
"Serikali imepata pigo kubwa kwa sababu inawekeza pesa nyingi katika kuwasomesha wanafunzi kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya juu kwa kuwapa mikopo."
FUNDISHO KWA MTUAkirejea agizo la Rais Magufuli la vyombo vya dola kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha tukio hili, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni alisema:
Uchunguzi utakapokamilika serikali itatoa taarifa ambayo itakuwa fundisho kwa mtu mwingine kusababisha hali kama hiyo kutokea tena. Aidha, Masauni alisema siasa isiwe chanzo cha watu kufariki au kuwa walemavu.
Alisema serikali kwa sasa inataka kujiridhisha undani wa tukio hilo lilivyotokea bila ya kumuonea mtu yoyote, na kwamba uchunguzi hautachukua muda mrefu.
"Nani anajua ile risasi ilitoka kwa nani? Kama yupo anayejua aje atuambie, kwa sasa maiti ipo hospitali tunasubiri taarifa, hatuwezi kukurupuka tu," alisema Masauni.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lilishasema mapema jana linawashikilia askari wake sita kufuatia tukio hilo na silaha zao zinachunguzwa, ikiwa ni pamoja na kuzipeleka kwa wataalamu wa milipuko kwa uchunguzi wa kina.
Aidha, jeshi hilo lilisema limeunda timu ya upelelezi ili kuchunguza chanzo cha kifo cha binti huyo.