Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Amana wilayani Ilala umemuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kusaidia mchakato wa kulipata jengo la Amana Center ili litumike kupunguza uhaba wa majengo unaoikabili hospitali hiyo.
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Meshack Shimwela ametoa ombi hilo leo Februari 14,2018 wakati wa uzinduzi wa jengo la huduma ya mama na mtoto hospitalini hapo.
Amesema wamekuwa na mzozo wa mara kwa mara na watumiaji wa jengo la Amana Center kutokana na upigwaji wa muziki na burudani nyingine za sanaa.
Dk Shimwela amesema jengo hilo lipo karibu na hospitali na kelele zinasumbua wagonjwa, hivyo ameiomba Serikali ione umuhimu wa kuwapa jengo hilo ambalo wameliomba kwa muda mrefu.
Amesema hospitali hiyo hupokea wagonjwa kati ya 180 na 250 kwa siku, miongoni mwao wakiwa ni wajawazito ambao wanaojifungua kwa siku ni kati ya 60 na 100.
Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu amesema Hospitali ya Amana imeomba jengo hilo linalomilikiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na taarifa za maombi zimefika hadi kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, hivyo Serikali ione haja ya kujibu maombi hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akisisitiza umuhimu wa Serikali kukabidhi jengo hilo kwa hospitali, amesema anaamini waziri mkuu anaweza kusaidia jengo hilo kukabidhiwa kwa Amana hata kabla ya Ijumaa Februari 16,2018.
Waziri Mkuu, Majaliwa akijibu ombi hilo ameagiza ofisa ardhi wa Wilaya ya Ilala kufanya tathmini ya majengo yanayoizunguka hospitali hiyo, ikiwa ni pamoja na kufahamu gharama za fidia zitakazohitajika ili kuruhusu upanuzi.
“Nimepokea ombi lenu, mkuu wa mkoa amesema kwa spidi mliyonayo nitashangaa kama itafika siku ya Ijumaa kwa kuchomeka chomeka huyu, wewe sema hospitali inahitaji hilo jengo,” amesema waziri mkuu.
Amesema kabla ya kutoa uamuzi wowote anahitaji kujiridhisha kuhusu mmiliki wa jengo na matumizi yake, ingawa ni wazi kwamba matumizi ya hospitali ni muhimu.
Dk Shimwela akizungumzia jengo jipya, amesema litaongeza idadi ya akinamama wanaohudumiwa kutoka 253 wa sasa hadi 353.
Amesema kutokana na huduma za afya za kisasa zitakazotolewa kupitia jengo hilo, zitapunguza idadi ya vifo vya akinamama kutoka 18 hadi 14.
Amesema kwa utaalamu mama aliyejifungua hutakiwa kuwa chini ya uangalizi wa wataalamu wa afya kwa saa 24 lakini kutokana na uhaba wa vitanda wengine huruhusiwa mapema.
Dk Shimwela amesema changamoto nyingine inayowakabili ni upungufu wa watumishi ambao wapo 392 (sawa na asilimia 46) wakati mahitaji ni watumishi 671.
Uongozi wa Hospitali ya Amana Wamuomba Waziri Majaliwa Jengo la Amana Center
0
February 14, 2018
Tags