Uongozi wa klabu ya Ruvu Shooting kupitia kwa msemaji wake Masau Bwire umemuomba radhi mshambuliaji wa Simba Emmanuel Okwi kufuatia kufanyiwa tukio lisilo la kiungwana na mchezaji wao Mau Bofu.
Masau Bwire amesema wao kama uongozi wa Ruvu Shooting, pamoja na mchezaji mwenyewe wamekiri kufanya kosa hilo na wanamuomba radhi Okwi mwenyewe, uongozi wa Simba pamoja na wapenda soka wote.
Bofu alimpiga kiwiko Okwi katika dakika ya 43 ya mchezo kati ya timu hizo siku ya Jumapili wikiendi iliyopita, kwenye Uwanja wa Uhuru, ambapo mwamuzi alimtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja licha ya kuwa tayari alikuwa na kadi ya njano.
Kitendo hicho kilisababisha Okwi asiendelee na mchezo hivyo kulazimika kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Laudit Mavugo. Katika mchezo huo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0.
Okwi anaongoza orodha ya wafungaji msimu huu akiwa na mabao 12 hadi sasa, wakati klabu yake ya Simba ikiwa kileleni mwa msimamo ikiwa na alama 38.