Uongozi wa Jiji la Entebbe nchini Uganda umeifunga Baa ya De ambayo mwanamuziki Moses Ssekibogo maarufu kwa jina ‘Mowzey Radio’ alikuwapo na kujeruhiwa wiki mbili zilizopita.
Mwanamuziki huyo alifariki dunia jana katika Hospitali ya Case alipokuwa akipatiwa matibabu.
Gazeti la Daily Monitor nchini humo limeripoti kuwa agizo la kufungwa kwa baa hiyo limetoka kwa Meya wa Jiji, Paul Kayanjana.
Mbali na kuchukua hatua hiyo, Meya Kayanjana ameagiza apelekewe vibali vyote vya baa hiyo ikiwamo leseni na kuwekwa makufuli katika milango yote.
Hata hivyo, ameonya kuwa endapo mmiliki wa baa hiyo atakaidi amri hiyo ya kutoendelea na uendeshaji atatozwa faini ya Sh1milioni za Uganda ambazo atapaswa kuzilipia kupitia Benki ya Stanbic, Tawi la Entebbe.
Katika hatua nyingine, watu wameonekana kuzidi kumiminika katika ukumbi wa Taifa wa maonyesho ambako wananchi watauaga mwili kabla ya maziko yatakayofanyika kesho saa 10 jioni Kaga, Barabara ya Entebbe.
Mwanamuziki Radio aliyewahi kutamba na kundi la Goodlyfe alilazwa katika Hospitali ya Case baada ya kushambuliwa katika ugomvi uliotokea wiki mbili zilizopita katika Baa ya De.
Ugomvi huo unaodaiwa kuwa kati yake na mlinzi wa baa hiyo, ulimsababishia apasuke fuvu na kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa wiki mbili.