Wakili wa serikali Vitalis Peter amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi hiyo imeitishwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba jalada bado lipo kwa (DPP) kwa ajili ya kulipitia na kulitolea maamuzi.
Baada ya kusema hayo Hakimu Simba amesema kesi hiyo sio suala la upande wa mashtaka kuamua wanavyotaka na kwamba hataki kesi hiyo ifike miaka mitatu kama kesi nyingine zilizopo.
“Hakikisheni upelelezi unakamilika haraka kesi hii isichukue muda mrefu kama nyingine kwani jamii inajua Mahakama ndio inachelewesha kesi” -Hakimu Simba
Hakimu Simba aliutaka upande wa mashtaka wakati ujao wawe na lugha inayoeleweka la sivyo kuna kitu atakifanya na wakae wakijua washtakiwa wapo ndani.
Naye Wakili wa utetezi Alex Mgongolwa amedai hawajaenda mahakamani kutembea na kuiomba mahakama iamuru upande wa mashtaka kutekeleza majukumu yao na haki iweze kutendeka.
Awali jalada hilo lilipelekwa kwa DPP ambapo alilipitia na kulirejesha TAKUKURU na kuelekeza baadhi ya maeneo yafanyiwe uchunguzi zaidi.
Hakimu Simba aliiahirisha kesi hiyo hadi March 6,2018 na kuutaka upande wa mashtaka uhakikishe wanalifanyia kazi jalada hilo.
Mbali na Gugai, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni George Makaranga, Leonard Aloys na Yasini Katera.
Washtakiwa hao wanaokabiliwa na mashtaka 43 yakiwemo 20 ya utakatishaji fedha haramu, kumiliki mali zisizoendana na kipato na kughushi mikataba ya mauziano ya viwanja katika maeneo mbalimbali.