Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo, Maria Mashingo amesema vifaranga vya kuku 5,000 vilivyokamatwa katika mpaka wa Namanga vikiingizwa nchini kwa njia isiyo halali vimeharibiwa.
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi jana, Mashingo hakufafanua jinsi vifaranga hivyo vilivyoharibiwa.
“Sheria za kimataifa ziko wazi, zinasema kama hakuna utambulisho wa bidhaa zinapaswa kuharibiwa, hatujui ubora wake kwa kuwa aliyekuwa akivisafirisha hakuwa na taarifa. Hakuna haja ya kuumiza sekta nzima ya kuku kisa vifaranga 5,000 tu,” alisema Mashingo.
Alisema licha ya kukosekana kwa taarifa za vifaranga hao, pia mmiliki wake hakuwa na kibali cha kuvisafirisha, hivyo sheria ilichukua mkondo wake.
Awali, meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika mpaka wa Namanga, Edwin Iwato alisema baada ya kukamatwa vifaranga hivyo mwishoni mwa wiki vikiingizwa nchini kutoka Kenya, mamlaka ilivikabidhi kwa maofisa wa Wizara ya Mifugo. “Kuhusu kuteketezwa vifaranga kama tulivyofanya kwa vya awali 6,400, sasa wenye jukumu hilo ni Wizara ya Mifugo,” alisema Iwato alipoulizwa jana kuhusu vifaranga hivyo.
Oktoba mwaka jana vifaranga vya kuku 6,400 vilikamatwa mpakani Namanga vikiingizwa nchini kutoka Kenya na baadaye viliteketezwa kwa moto.
Kuteketezwa kwa vifaranga hivyo vilivyokuwa na thamani ya Sh12.5 milioni mali ya mfanyabiashara Mary Matia (23) mkazi wa Mianzini jijini Arusha kuliibua mjadala nchini. Mamlaka inayohusika na udhibiti wa magonjwa ya mifugo Kanda ya Kaskazini ilisema viliteketezwa kwa kuzingatia Sheria ya Magonjwa ya Wanyama namba 17 ya mwaka 2003.
Ilielezwa pia kuwa Serikali mwaka 2007, ilitoa tangazo kupiga marufuku kuingizwa nchini vifaranga vya kuku na mayai.
Baada ya kuteketezwa vifaranga hivyo, Serikali ya Kenya ilifanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini humo, Pindi Chana kutafuta suluhu ya vikwazo vya kibiashara vilivyopo baina ya mataifa haya jirani.