Vigogo saba wa madini ya Tanzanite katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro na jijini Arusha, waliokuwa wanashikiliwa na Polisi kwa amri ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti wakidaiwa kudhamini uchimbaji haramu wa madini hayo, wameachiwa kwa dhamana.
Akizungumza jana, Februari 12, 2018 na MCL Digital, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Agustino Senga amesema vigogo hao waliokuwa wanashikiliwa kwenye kituo cha polisi Mirerani wamepatiwa dhamana, lakini bado polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Wiki iliyopita Mnyeti aliagiza vigogo hao saba wa madini kukamatwa na kushikiliwa kwenye kituo cha polisi Mirerani wakidaiwa kufadhili uchimbaji huo haramu.
Amesema waliwashikilia wachimbaji hao baada ya kamati iliyoundwa na Mnyeti kupata taarifa kuwa vigogo hao wanashiriki kuwadhamini vijana wanaoingia kwa wizi kwenye migodi ya kampuni ya TanzaniteOne yenye ubia na Serikali kwa asilimia 50 kwa 50 na Shirika la Madini la Taifa (Stamico).
Amesema wamewapatia dhamana vigogo hao (majina yao tunayahifadhi kwa sasa) ila bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
"Bado tunaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kwani watuhumiwa hao wanadaiwa kuwadhamini wachimbaji hao haramu ambao wanaingia migodini bila uhalali," amesema Senga.
Amesema kuna kamati maalumu iliundwa na mkuu wa mkoa huo kwa ajili ya kuchunguza suala hilo hivyo baada ya uchunguzi wa awali ikabidi vigogo hao wakamatwe.
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Manyara (Marema), Sadiki Mneney amesema wao kama chama bado hawajatambua sababu ya kukamatwa kwa wachimbaji hao.
Mneney amesema baada ya wachimbaji hao kuachiwa kwenye kituo cha polisi Mirerani walipanda magari yao na kuondoka, hivyo bado hawajazungumza nao.
"Tumepata taarifa kuwa wameachiwa ila viongozi tulipanga kufuatilia jambo hili mjini Babati kwani tulikuwa hatujui ni sababu gani iliyofanya wachimbaji hao wa madini kushikiliwa kwenye kituo cha polisi," amesema Mneney.