Viongozi wa Chadema Wavamia Ofisi za Tume ya Uchaguzi Kudai Viapo vya Mawakala Wao

Viongozi wa Chadema Wavamia Ofisi za Tume ya Uchaguzi Kudai Viapo vya Mawakala Wao
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wengine wa chama hicho wamekwenda makao makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kudai viapo vya mawakala wa chama hicho katika uchaguzi wa ubunge jimbo la Kinondoni.

Baada ya kufika katika ofisi hizo leo Februari 15, 2018 saa 6:30 mchana, Mbowe na viongozi hao wamekwenda moja kwa moja katika ofisi za Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima.

Awali Mbowe amewaeleza waandishi wa habari waliopo katika ofisi hizo kuwa licha ya kumpigia simu ya mkononi Kailima hampati, baadaye kubainisha kuwa ameelezwa na mkurugenzi huyo kuhorodhesha madai yao na kumpa taarifa.

“Tumekubaliana naye katika hilo na nimewaita wabunge tumeingia kwenye chumba maalum hapa NEC ili kuoroshesha madai yetu,” amesema.

Amesema baada ya kuorodhesha watawasiliana na Kailima na kwamba amewaahidi kuyatafutia ufumbuzi malalamiko yao leo.

Februari 10, 2018 Chadema na CUF vilidai kuwepo kwa njama jimbo la Kinondoni baada ya mawakala wao kulazimishwa kula kiapo bila kukabidhiwa viapo vyao.

Madai hayo yalitolewa na mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kinondoni, Waziri Muhuzi na mkurugenzi wa habari, uenezi na uhusiano wa umma wa CUF, Abdul Kambaya, kubainisha kuwa endapo viapo havitatolewa katika muda muafaka mawakala wao wanaweza kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kusimamia kura za ubunge na udiwani.

Hoja tano za Chadema dhidi ya Nec

Mbowe amesema malalamiko ya Chadema kwa NEC ni; Mosi, mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni kukataa kuwaapisha mawakala wa ziada, kwamba vituo vipo 613 na amewaapisha mawakala 613.

Pili, ni Kailima kukataa wabunge na madiwani wa Chadema kuwa mawakala; tatu, Kailima kuja na sharti jipya kutaka mawakala wote wawe na vitambulisho; nne, kutotolewa kwa hati za viapo kwa mawakala hadi sasa; tano,  kituo cha majumuisho ya kura hakifahamiki.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad