Viongozi dini na wanasiasa wamepanga kwenda kumuona Rais John Magufuli wakiwa na pendekezo la kukamilishwa kwa mchakato wa kupatikana Katiba Mpya.
Azimio hilo limefikiwa kwenye kongamano la viongozi wa siasa na wa dini lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), lililofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Mbatia alisema lengo la kongamano hilo ilikuwa kujadili hali ya nchi kutokana na hofu iliyomo miongoni mwa wananchi, huku kukiwa na malalamiko ya ukandamizwaji wa demokrasia kutoka kwa vyama vya siasa.
Akisoma mapendekezo ya mkutano huo, Mwenyekiti wa TCD ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR -Mageuzi, James Mbatia alisema pia kuna haja ya kujenga taasisi imara za usawa na haki.
Mbatia alisema mapendekezo mengine ni kuimarishwa uhuru wa kutoka maoni na kuwataka wadau wa siasa kujiepusha na siasa za chuki.
Hata hivyo, mwakilishi wa CCM, Wilson Mukama akizungumza na Mwananchi baada ya kumalizika kongamano hilo alisema Katiba Mpya si kipaumbele cha Serikali ya sasa.
Mukama aliyewahi kuwa katibu mkuu wa chama hicho alitoa mfano wa Kenya akisema licha ya kuwa na katiba mpya imeendelea kuwa na vurugu.
Wakizungumza nje ya ukumbi kutokana na waandishi wa habari kutoruhusiwa katika kongamano hilo, Amir wa Shura ya Maimamu nchini, Alhaj Sheikh Musa Kundecha alisema Jeshi la Polisi linatumia nguvu kubwa hali inayotia hofu wananchi.
Kuhusu mfumo wa demokrasia, alisema kumekuwa na ukandamizwaji wa vyama vya upinzani wakati vipo kisheria.
Askofu Benson Bagonza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera alisema kinachohitajika sasa ni kuwa na siasa shirikishi bila kujali jinsi na vyama vya siasa.
Viongozi wa dini Mwanza
Wakati TCD na viongozi wa dini wakiazimia hayo Dar, mkoani Mwanza viongozi wa dini wameitaka Serikali kutimiza wajibu wa kulinda usalama wa raia na mali zao kwa kudhibiti vitendo vya watu kutekwa, kupotea na kuuawa vinavyoanza kushamiri.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana, viongozi hao wametaja kutekwa kwa baadhi ya wasanii, kupotea kwa mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Mwananchi, Azory Gwanda na vifo vya watu wawili wakati wa mchakato wa uchaguzi mdogo Jimbo la Kinondoni kuwa miongoni mwa mambo yanayotia doa Taifa.
Akisoma tamko la asasi za kiraia kuhusu hali ya usalama wa raia, haki za binadamu, na utawala wa sheria, Sheikh Mohammed Hassan alisema ni wajibu wa Serikali kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya watu kupotea na vifo vyenye utata.
Askofu Stephen Genga alisema, “Pamoja na kuomba Tanzania iwe Taifa lenye jamii yenye hofu ya Mungu; ni wajibu wetu viongozi wa dini kuonya na kukemea matukio ambayo si tu yanakiuka mafundisho ya dini zote, bali pia haki ya msingi ya binadamu ya kuishi.”
Tamko asasi za kiraia
Jijini Dar es Salaam, asasi 100 za kiraia zimetoa tamko likitaka mchakato wa Katiba Mpya ufanyike mwaka huu.
Akisoma tamko hilo, mkurugenzi wa shirika la Equality For Growth (EfG), Jane Magigita alisema Serikali itazame upya suala la upatikanaji wa Katiba Mpya kwa kuwa ndiyo suluhisho la matatizo yanayotokea kwa jamii.
“Suala la katiba limekuwa ni kilio kikubwa na hitaji la Watanzania wengi ili kutibu hali inayojitokeza. Tunashauri mchakato wa Katiba Mpya ufanyike mwaka huu kwa kuwa mwaka 2019 na 2020 Taifa litakuwa katika uchaguzi,” alisema.
Kuhusu upatikanaji wa fedha za kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya, mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Dk Hellen Kijo Bisimba alisema hilo lipo ndani ya uwezo wa Serikali kwa kuwa kuna mambo mengi imefanya ambayo hayakuwa ndani ya bajeti ya nchi na kwamba kuna haja ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kufungua ofisi zake wilayani na kuajiri wataalamu wa kusimamia uchaguzi na kuachana na mfumo wa sasa unaoonekana kuwa na mgongano wa kimasilahi.