Viongozi watano wa Dini ya Kiislamu wanadaiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha na Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (Jumaza) imeviomba vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa suala hilo.
Viongozi hao ni mlezi wa taasisi za Kiislamu, Amir Haji Khamis Haji mkazi wa Mpendae, Hamad Ali Haji mkazi wa Fuoni, Suleiman Juma Suleiman (Makadara), Salum Said Chande (Kinuni) na Abbas Said Chasuma wa Kizimbani.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali alisema jana kwamba hawajui walipo.
Awali, naibu katibu mtendaji wa Jumaza, Khamis Yussuf Khamis alisema kupotea kwa watu hao hakuleti taswira nzuri na kuvitaka vyombo kuliona hilo na kulifanyia kazi haraka.
Alisema kuwa vyombo hivyo ndivyo vyenye jukumu la kuhakikisha amani na haki za raia wote visiwani Zanzibar zinapatikana kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi.
Alisema Jumaza itaendelea kufuata taratibu za kisheria katika kuhakikisha waumini hao wa dini ya Kiislamu wanatafutwa hadi kupatikana ili kuzipa faraja familia na jamaa hao.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda Ali alisema Jeshi la Polisi linasikitishwa na tukio hilo na kuahidi kushirikiana na familia za waliopotelewa kuwasaka walipo.