Viongozi wa Serikali walio madarakani na wastaafu wakiongozwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wamejumuika na waombolezaji wengine kuaga mwili wa mwanasiasa mkongwe nchini, marehemu Kingunge Ngombale Mwiru.
Shughuli ya kuaga mwili wa Kingunge imefanyika leo Jumatatu Februari 5,2018 katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.
Viongozi wengine walioaga mwili wa Kingunge ni marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa aliyeambatana na mkewe Anna; Makamu wa Rais mstaafu, Dk Mohamed Gharib Bilal; mawaziri wakuu wastaafu Dk Salim Ahmed Salim, Frederick Sumaye, Edward Lowassa na mkewe Regina; na Jaji mstaafu Joseph Warioba.
Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula na mtangulizi wake Pius Msekwa; Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Othman Chande; Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Pia, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole; Mama Maria Nyerere; Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye; na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba.