Serikali imetangaza utaratibu mpya wa kuingia katika machimbo ya Tanzanite yaliyopo Mererani ambapo kuanzia Februari 15 ni lazima mtu awe na kitambulisho maalumu.
Akizungumza na wachimbaji wa madini hayo jana Februari 13 mjini hapa, Kamishna na Madini Kanda ya Kaskazini, Adam Juma alisema vitambulisho vitakavyotakiwa ni vile vinavyotolewa na Wizara ya Madini.
Juma alisema hadi sasa ni vitambulisho 6,000 ambavyo tayari vimetolewa na katika machimbo hayo kuna wachimbaji zaidi ya 15,000.
“Baada ya ujenzi wa ukuta kukamilika sisi kama wizara tutaanza Februari 15 kudhibiti kuingia migodini,” alisema.
Alisema wamiliki wa migodi yote, wachimbaji na madalali wa madini pamoja na watu wengine ambao watataka kuingia kwenye eneo lililozungushwa ukuta lazima wawe na vitambulisho.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula alisema agizo hilo la Serikali halina utani, hivyo ni lazima wanaotaka kuingia migodini wafuate sheria.
Alisema lengo ya mpango huo ni kuhakikisha madini hayatoroshwi na pia Serikali inapata stahiki zake kabla ya madini kutoka nje ya uzio.
Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Manyara (Marema), Sadiki Mnenei alisema wanaunga mkono mpango wa vitambulisho, lakini wanaomba muda zaidi wa kuzuia wasio na vitambulisho hadi Machi mosi.
“Ili kutoathiri kazi zetu tunaomba utaratibu mpya kuanza mwezi ujao kwani gharama za kitambulisho ni kubwa kwa kuwa kila mchimbaji anatakiwa kutoa Sh3,500 na mmiliki wa mgodi Sh5,000,” alisema.
Alisema kwa wastani mgodi mmoja una zaidi ya wafanyakazi 100, hivyo wote kuwapa vitambulisho wakati mmoja ni vigumu.