Wakazi Kinondoni Wajitokeza Kupiga Kura
0
February 17, 2018
Wakazi wa jimbo la Kinondoni wamejitokeza kupiga kura katika uchaguzi mdogo wa ubunge unaofanyika leo Februari 17,2018.
Timu ya waandishi wa MCL Digital iliyopiga kambi jimboni humo imebainisha kuwa idadi ya watu wanaojitokeza si kubwa kulinganisha na wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Vitu vya kupigia kura vimefunguliwa saa moja asubuhi, huku baadhi ya wapiga kura wanaonekana wakiangalia majina yaliyobandikwa vituoni kabla ya kupiga kura. Wengine wachache wameeleza kutoona majina yao.
Malalamiko ya mawakala
Iddy Ramadhani, wakala wa CUF kituo cha Minazini kilichopo Kata ya Mwananyamala ameieleza MCL Digital kuwa hadi saa mbili asubuhi hakuwa ameruhusiwa kuingia kituoni licha ya kuwa na barua ya utambulisho.
“Mimi ni wakala wa CUF na nina barua ya kiapo na karatasi ya chama inayonitambua kama wakala lakini wanakataa nisiingie ndani. Watu wanaanza kupiga kura wakati mawakala hawapo ndani hii si sahihi,” amesema Ramadhani.
Wakala mwingine wa Chadema katika kituo namba 3 kilichopo eneo la Serikali ya Mtaa Kijitonyama, Erasto Nicholaus amesema ameondolewa kituoni kwa sababu ya kutokuwa na barua ya kiapo.
Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko amesema jana usiku walifuatilia barua za viapo vya mawakala bila mafanikio kwa madai kuwa walizungushwa na watendaji wa ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni.
“Barua nimepewa saa 1:30 asubuhi na tatizo ni kwamba unampeleka wakala kituo kimoja lakini barua ya mkurugenzi inakuja na inasema wakala huyo aende kituo kingine,” amesema Matiko.
Licha ya changamoto hiyo, hali ya usalama ni shwari kutokana na polisi kuonekana vituoni wakiwa katika magari.
Jimbo la Kinondoni lina kata 10 na kati ya hizo, ya Makumbusho mwandishi wa MCL Digital ameshuhudia wanaojitokeza kupiga kura wakiwa wachache.
Msimamizi wa kituo namba 1 na 2 katika Mtaa wa Bwawani uliopo Kata ya Makumbusho, Allein Seth amesema, “Mpaka sasa kazi inakwenda vizuri na hakuna tatizo lolote licha ya mwitikio kuwa mdogo."
"Tuwaombe wananchi wa eneo hili wajitokeze kuja kumchagua kiongozi wao na wasibaki nyumbani na kuwaachia jukumu hili watu wengine kwa kuwa maendeleo yao yatategemea viongozi waliowachagua," amesema Seth.
Tags