Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla amewataka wamiliki na waendeshaji wa hoteli za daraja la kati kumwandikia mapendekezo yatakayomwezesha kutoa uamuzi sahihi wa namna wanavyoweza kuchangia mapato ya nchi.
Akizungumza jijini hapa leo Februari 9, Dk Kigwangalla amesema uchunguzi wao umebaini kuwa hoteli zenye hadi ya kati na nyumba za kulala wageni maarufu 'Guest House' zimekua zikipokea watalii wengi kutokana na ubora wake unaochangiwa na unafuu wa bei.
Amesema tafsiri ya watalii haimaanishi Wazungu pekee bali ni wageni wowote wanaotumia nyumba za kulala wageni kutoka nje ya eneo hilo wakiwemo wanaofika kwa ajili ya mikutano na shughuli za biashara.
''Mnaweza kuniambia hoteli zetu zina hadhi ya chini kwa sababu bei ya chumba ni kati ya Sh40,000 hadi 70,000 lakini tunafahamu hizi hoteli Wazungu wameshazijua na wanalala kwenye hoteli zenu na mnaweza kuanza kuwatoza kwa dola,"amesema Kigwangalla.
Amesema lengo la Serikali ni kuwawezesha kukusanya mapato yanayosaidia kuipa uwezo wa kuwahudumia wananchi kwenye sekta mbalimbali zikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya barabara, usambazaji wa huduma ya maji, elimu na afya.
Mmoja wa wamiliki wa hoteli hizo, Amani Charles amesema wanakusudia mapendekezo watakayowasilisha kwa Dk Kigwangalla baada ya kukubaliana yatawawezesha kufanya biashara kwa njia nzuri badala ya kunyonywa kimapato kutokana na kutokuwepo usawa wa malipo.
Amesema mkanganyiko wa malipo unatokana na wao kutakiwa kulipa kwa dola ya Marekani 1.5 kwa kitanda ambayo ni karibu Sh2,000 wakati wateja wao wanalipa kwa fedha za Kitanzania huku uamuzi wa kulipa kwa kiwango maalumu kwa mwaka au kwa asilimia kulingana na wateja wanaolala.
Naye Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amesema utaratibu ambao umeshawekwa na Mamlaka ya mapato(TRA) mkoa wa Arusha utaendelea kwa sababu Serikali imeshaweka malengo ya makusanyo na wale ambao ukadiriaji wa mapato yao umefanyika hivi karibuni utapatiwa majibu na Waziri wa Maliasili na Utalii.