Jana haikuwa siku nzuri kwa mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Aaron Mbogho baada ya wananchi kumshtaki kwa mkuu wa mkoa wakisema ameshindwa kutatua kero ya maji.
Katika kuonyesha ukubwa wa kilio chao, baadhi yao walimuomba mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira kuvaa kofia ya mkuu huyo ili awatumikie.
Wananchi wa kata za Toloha na Kiria wilayani Mwanga walieleza hayo juzi wakisema tangu Mbogho ateuliwe na Rais kuongoza wilaya hiyo hawajawahi kumwona katika maeneo yao akifuatilia changamoto zinazowakabili.
Katika mikutano iliyofanyika kwenye kata hizo kwa nyakati tofauti, wananchi hao walilalamikia kero mbalimbali lakini kubwa ikiwa ni ya maji.
Mkazi wa Kata ya Kiria, Ayubu Msangi alimuomba Mghwira aifanye Wilaya ya Mwanga iwe Moshi ili aweze kutatua kero zinazowakabili.
“Hatumtaki mkuu wa wilaya, ana dharau, hatufai kabisa, utakapochukua kero zetu na kuziacha ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Mwanga wataacha palepale bila kuzifanyia kazi na kukudharau. Tunataka wilaya yetu sasa iwe ya Moshi ili tukipata tabu tukueleze wewe mama na mkuu wa wilaya yetu utakua ni wewe kuanzia leo,” alisema Msangi.
Msangi alisema wanapopeleka malalamiko kwenye ofisi za ngazi ya wilaya hakuna kinachotekelezeka, badala yake inayakumbatia.
Alisema kwa muda wa wiki mbili sasa, maji hayapatikani katika Kata ya Kiria hali ambayo inawalazimu kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 13 kutafuta ndoo moja ya maji.
“Tatizo hili ni kubwa maana linaharibu shughuli za uchumi, tunaomba hatua ya haraka ichukuliwe. Wananchi wanashindwa kufanya shughuli yoyote kama tunavyojua, maji ni uhai,” alisema.
Jane Mkwizu mkazi wa Kijiji cha Kizungo kilichopo Kata ya Toloha alisema wanakwenda kutafuta maji mbali kuanzia saa kumi na moja asubuhi hadi saa 10 jioni ndipo huyapata na hujikuta wakirejea nyumbani saa mbili usiku.
“Tunaomba mama utusaidie. Wewe ni mwanamke mwenzetu, tunaomba usikie kilio chetu utufuatilie kama hayo maji yatarudi maana tumerudi kwenye umaskini ambao tulitoka miaka ya nyuma wakati wenzetu wanapiga hatua,” alisema.
Baada ya kusikiliza malalamiko hayo ya wananchi, Mghwira hakumpa nafasi mkuu wa wilaya kuzungumza badala yake, alimuagiza mhandisi wa maji Wilaya ya Mwanga, Ernesta Kihwele kufunga mabomba yote yaliyoungwa holela kwenye chanzo cha maji kilichopo Msitu wa Kindoroko.
“Naomba kuanzia sasa mabomba yote yakafungwe kwenye vyanzo vya maji isipokuwa mabomba yanayopeleka maji kwenye huduma za afya ili wananchi wa Toloha wapate maji hadi matangi yenu yajae ndipo mgao uanze,” alisema Mghwira.
Mkuu wa mkoa alisema mgao huo ukisimamiwa vizuri, maji yatapatikana kwa wote bila adha yoyote.
Mbali ya kero ya maji, wananchi wa Kata ya Kiria waliilalamikia halmashauri ya wilaya hiyo kwa kushindwa kutengeneza miundombinu ya barabara licha ya wakulima kutozwa Sh2,000 kwa gunia moja wanapotoa mazao shambani.
Mkuu wa wilaya ajitetea
Akizungumza kwa simu jana kuhusu malalamiko ya wananchi, Mbogho alisema hayana msingi kwa kuwa kila kitu huwa kinafanyika kiutaratibu na kwa mipango iliyopangwa kwa wakati.
“Mtu aje ofisini tujue tatizo lake liko wapi, kwani kuna mtu aliwahi kuja ofisini akafukuzwa? Kila kitu kinafanyika kiutaratibu na tunafanya vitu ambavyo viko kwenye bajeti,” alisema.
Mbogho alisema hawezi kuzungumzia kitu ambacho ni cha jumla jumla na pia hawezi kufanya kitu kilicho nje ya mstari.