Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amefunguka na kuwataka watumishi mbalimbali mkoani kwake ambao hawaiungi mkono Serikali ya awamu ya tano iliyopo chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuondoka mapema katika nafasi zao hizo.
Mnyeti amesema kuwa siku zote Chama Cha Mapinduzi ndiyo kimekuwa kikihangaika kuomba kura majukwaani huku viongozi mbalimbali wa chama hicho wakiwa si wanufaika wakubwa kulinganisha na watumishi, hivyo watumishi wanapaswa kutambua na kuiunga mkono Serikali ya CCM na kama hataki waondoke kwenye nafasi hizo.
"Wanaoumia kuomba kura majukwaani ni CCM anayekuja kula ugali na familia yake ni wewe mtumishi, unanufaika wewe na familia yako. Sasa tumejipanga vizuri wale wote ambao siyo wenzetu watupishe mapema kabla ya uchaguzi, mimi ndiyo Mkuu wa Mkoa huu wa Manyara nasema hivi kama wewe huungi mkono Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ondoka mapema" alisisitiza Mnyeti