Mkuu wa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Rehema Madusa, ameliagiza Jeshi la Polisi wilayani humo kuwakamata na kuwapa adhabu ya kufyatua tofali vijana wanaovaa mavazi yasiyokuwa na staha hadharani.
Bi. Madusa ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika stendi ya mabasi wilayani humo ambapo amesema tofali hizo zitatumika kuboresha makazi ya askari.
Aidha amesema dawa imepatikana kwa baadhi ya vijana wa kike ambao wamekuwa wanavaa nusu uchi hadharani na wanaume wanaovalia mlegezo na kuagiza wakamatwe na waoneshwe sehemu ya kufyatulia matofali yatakayotumika kwa ajili ya ujenzi wa vyoo na nyumba za polisi.
“Hawa wanaotembea barabarani nusu uchi basi wakiona vizuri basi watoe zote watembee uchi kabisa tujue moja, jeshi la polisi kamateni watu hawa pelekeni waende wakafyatue tofali kwa ajili ya kujenga nyumba za polisi,” Madusa
Hata hivyo amesema hata wanaokunywa pombe nyakati za kazi na wale wanaopiga debe bila kufuata utaratibu uliowekwa wataunganishwa pamoja kusaidia kufyatua tofali hizo.
“Wote hawa mimi nawaweka katika kundi moja kuanzia wacheza pool table, wapiga debe wanaovaa nguo zisizokuwa na staha na wale wanaovaa nguo nusu uchi, naagiza polisi na wananchi kamateni hawa wakasaidie ujenzi,”amesema.
Hata hivyo ameliagiza jeshi la polisi kushirikiana na wananchi kudhibiti matukio ya uhalifu ikiwemo vitendo vya ujambazi na usalama barabarani.