Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hali ya usalama wa chakula nchini imeimarika kutokana na uzalishaji mzuri wa mazao ya chakula.
Waziri Majaliwa ameyasema hayo wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 10 wa Bunge la 11 mjini Dodoma Bunge na kutaja mazao hayo kuwa ni pamoja na mahindi yaliyovunwa katika mikoa ya Ruvuma, Njombe, Iringa, Katavi, Kigoma, Mbeya, Songwe na Rukwa.
"Matarajio yetu kuwa hali ya mavuno msimu huu itakuwa nzuri kwa sababu mwenendo wa unyeshaji wa mvua za vuli ulikuwa wa kuridhisha katika maeneo mengi nchini. Serikali inaendelea kusimamia na kuhakikisha kuwa hali ya utengamano na usalama wa chakula unaendelea kuwa imara kwa wananchi wote na kwa wakati wote", amesema Waziri Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu amesema serikali inawezesha wafanyabiashara wa mazao ya chakula kuendelea kusafirisha na kuuza mazao ya chakula nje na ndani ya nchi.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema upatikanaji na usambazaji wa pembejeo kwa wakulima umeimarika, ambapo takwimu zinaonesha kwamba hadi kufikia Februari Mosi, 2018 upatikanaji wa mbolea nchini kwa ajili ya mahindi na tumbaku ulifikia tani 250,376 sawa na asilimia 51.6 ya wastani wa mahitaji ya tani 485,000 kwa mwaka.
Waziri Majaliwa: Hali ya Usalama wa Chakula Nchini Imeimarika
0
February 10, 2018
Tags