Waziri Ummy Eeleza yaliyomkuta Aliyekuwa Mkurugenzi Benki ya Wanawake
0
February 06, 2018
Dodoma. Watumishi 20 akiwamo aliyekuwa mkurugenzi wa Benki ya Wanawake Tanzania (TWB), Magreth Chacha wamefikishwa katika vyombo vya uchunguzi kwa lengo la kuangalia uwezekano wa kuwashtaki kutokana na kuitia hasara benki hiyo.
Kauli hiyo imetolea leo Februari 6, 2018 bungeni mjini Dodoma na waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na kwamba watumishi hao wanachunguzwa na Takukuru na Polisi.
Amesema mkurugenzi huyo amekabidhiwa katika vyombo hivyo tangu Julai mwaka jana.
“Tuliamua kumpeleka Magreth na watumishi wengine jumla wapo 20. Vyombo vyetu vinawachunguza maana kumekuwa na tatizo kubwa katika benki hiyo ikiwamo kukopesha Saccos, lakini uchunguzi unaonyesha hakuna hata mtu mmoja aliyekopa,”amesema Ummy.
Waziri huyo alikuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa viti maalumu (CCM), Faida Mohammed Bakari aliyehoji hatua zilizochukuliwa kwa watu waliohujumu benki hiyo aliyodai imeshindwa kutimiza wajibu wake.
Katika swali lake la msingi, Faida alitaka kujua ni lini TWB itaanzisha tawi lake Zanzibar kwa ajili ya kuwapatia huduma za mikopo yenye riba nafuu na kuwainua kiuchumi wanawake wa Zanzibar.
Akijibu swali hilo la msingi, naibu waziri wa Afya, Dk Faustine Ndungulile amesema benki hiyo iliyoanzishwa mwaka 2009, lengo lake lilikuwa kuwakwamua wanawake na umaskini kwa masharti nafuu.
Dk Ndugulile amesema mpango wa benki hiyo ni kuhakikisha huduma zake zinawafikia wanawake mikoa yote ya Tanzania, ikiwamo Zanzibar kulingana na upatikanaji wa mtaji.
Mwananchi
Tags