Wiki moja baada ya akaunti ya Mtandao wa Kijamii wa Instagram ya Miss Tanzania 2006/07, Wema Isaac Sepetu kudukuliwa na wajanja wa mjini, mrembo huyo anadaiwa kupigwa mamilioni.
Habari zilizolifikia dawati la Gazeti la IJUMAA zilieleza kuwa, tangu mrembo huyo adukuliwe akaunti yake yenye wafuasi zaidi ya milioni tatu, wajanja hao wamekuwa wakiitumia ndivyo sivyo kwa kuposti matangazo mbalimbali ya kibiashara ambapo wanachukua pesa bila ya Wema kujua.
Inaelezwa kuwa, Wema alikuwa akitumia akaunti hiyo kupitia namba ya simu ya mtandao maarufu wa mawasiliano nchini ambapo wadukuzi walifanikiwa kumiliki namba hiyo ambayo hutumia moja kwa moja kuwasiliana na wafanyabiashara mbalimbali wa mtandao kwa mgongo wa Wema na kuvuna pesa.
Wema Sepetu akiwa kwenye pozi.
Wajanja hao, kwa siku moja tu hutumia akaunti hiyo kuvuna zaidi ya laki saba ambapo kwa wastani wa tangazo moja huchukua kiasi cha shilingi elfu hamsini hadi laki moja.
WATAALAMU WANASEMAJE?
Juma Abdul ambaye ni mtaalam wa masuala ya mtandao aliliambia Ijumaa kuwa, kwa hesabu ya haraka, tangazo moja hudumu kwa saa moja hadi tatu kutegemeana na maelewano ya mteja.
“Kwanza wale wateja wanaotuma matangazo, wengi hufanya makubaliano kupitia Direct Messages (DM) ambapo huamini wanawasiliana na mhusika mwenyewe (Wema) na hutumia namba yake ya simu kumtumia pesa bila kujua kuwa ni wadukuzi.
…Akifanya yake.
“Katika makubaliano hayo, huenda yanakuwa kwa saa au hata siku nzima kutegemeana na kiasi walichoafikiana na kwa hesabu ya haraka ni laki saba hadi nane kwa siku. Kwa hiyo kwa wiki nzima tangu wameanza kutumia akaunti yake wamefanikiwa kujipatia kuposti zaidi ya matangazo hamsini ambayo kimahesabu ni zaidi ya milioni 20,” alisema Juma.
WEMA ASAKWA
Ijumaa lilifanya jitihada za kumtafuta Wema kujua nini hatma ya akaunti hiyo ambayo inampotezea zaidi ya mamilioni tangu imedukuliwa ambapo simu yake iliita bila majibu.
Hata hivyo, alitumiwa ujumbe mfupi wa maneno ulioonesha wazi kumfikia lakini hakujibu.
MENEJA WAKE HUYU HAPA!
IJUMAA lilifanikiwa kumpata Meneja wa Wema, Neema Ndepanya na baada ya kuelezwa taarifa hizo alifafanua kuwa, jambo hilo lipo mikononi mwao na kwamba kuna vijana wawili wanaofanya kazi kwa ukaribu na Wema, Bestizo na mbunifu wa mavazi, Martin Kadinda ambao wanafuatilia kwa ukaribu.
“Ni kweli kabisa mpaka sasa Bestizo na Kadinda wanafuatilia kwenye mtandao wa simu (anautaja) kujua kwa nini wameshindwa kuthibiti suala hilo hadi sasa ambapo matapeli wanatumia njia kuwaibia watu kupitia akaunti hiyo,” alisema Neema.