Yanga Sasa Yachoka Majeraha ya Ngoma Yaandaa Kamati ya Kumtema

Yanga Sasa Yachoka Majeraha ya Ngoma Yaandaa Kamati ya Kumtema
NI wazi sasa klabu ya Yanga imechoshwa na hali ya majeraha ya muda mrefu kwa mchezaji wake, Donald Ngoma, na sasa klabu hiyo inafikiria kusitisha mkataba na Mzimbabwe huyo, imeelezwa.
Katibu Mkuu wa Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, Charles Mkwasa, akizungumza jijini Dar es Salaam jana, alikiri kuwa nyota huyo amekuwa majeruhi wa mguu kwa muda mrefu na kwa sasa klabu hiyo inafikiria kuhitimisha mkataba wake kama itaonekana hataweza kurejea uwanjani hivi karibuni.

"Ipo kamati itafuatilia kwa karibu mustakabali wa afya yake, huwezi kumlipa mshahara mchezaji ambaye haitumikii klabu, tutafuatilia kwa karibu afya yake kwa kupitia ripoti ya madaktari na baadaye tutajua nini cha kufanya," alisema Mkwasa.

Mkwasa, alisema wachezaji wengine ambao walikuwa majeruhi wamepata ripoti zao na wanaendelea vizuri akiwamo Thaban Kamusoko na Amissi Tambwe.

Kauli hiyo ya Mkwasa, iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Hussein Nyika, ambaye alisema ndani ya siku mbili watatoa msimamo wao juu ya mshambuliaji huyo mara baada ya kupokea taarifa ya madaktari.

"Ndani ya siku mbili tutajua nini cha kufanya, hatuwezi kukatisha ghafla mkataba wa mchezaji, tunasubiri ripoti ya madaktari kufahamu nini cha kufanya kama tutaambiwa hawezi (Ngoma) kurejea uwanjani hivi karibuni, hapo tutaangalia mengine kwa sababu huwezi kumlipa mshahara mchezaji ambaye hawezi kuitumikia klabu, analipwa kutokana na kucheza," alisema Nyika.

Ngoma, amekuwa na kipindi kigumu msimu huu baada ya kukosa sehemu kubwa ya msimu huu mpaka sasa, licha ya awali kuelezwa kuwa amepona majeraha yake wakati alipokwenda kujitibia nyumbani kwao Zimbabwe, na badala yake alicheza mechi tatu tu kabla ya kujitonesha tena na kukaa nje mpaka sasa.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad