Suala la mchezaji Donald Ngoma limebaki kiporo tena baada ya uongozi wa klabu ya Yanga kushindwa kufikia maamuzi pamoja na siku za hivi karibuni kuahidi kulishughulikia.
Akiongea leo Afisa habari wa Yanga Dismas Ten amesema taarifa ya awali kutoka ofisi ya katibu mkuu wa klabu hiyo Charles Mkwasa, kuwa suala la Ngoma linafanyiwa vikao jambo hilo limeshindwa kukamilika.
''Ukaribu wa michezo na majukumu mengi hapa katikati umefanya kushindikana kufikiwa kwa kile kilichokuwa kimepangwa au kulichotakiwa kujadiliwa kuhusiana na mchezaji huyo'', amesema.
Aidha Ten pia ameongeza kuwa majeraha kwa wachezaji hayazuiliki na pia wapo wachezaji waliokaa nje kwa muda mrefu na wakarejea wakasaidia timu zao hivyo Donald yupo ni mchezaji wa Yanga mpaka hapo taarifa nyingine itakapotolewa.
Kwa upande wake daktari wa timu hiyo Yanga Dr. Bavu amesema Ngoma ni miongoni mwa wachezaji wanne ambao bado ni majeruhi. Hivi karibuni Yanga walitoa taarifa kuwa wanasuburi ripoti ya dakatari juu ya afya ya Ngoma ili waweze kutoa uamzi.