KAZI imeanza! Kocha Mkuu wa Yanga, Mzambia, George Lwandamina, amesema hawatacheza soka la kujilinda katika mchezo wa leo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya St. Louis na badala yake watashambulia kuanzia dakika ya kwanza ili kumaliza mechi hiyo mapema.
Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Michezo ya Kubashiri Matokeo ya Sportpesa, jana ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana tayari kwa mchezo huo wa kwanza wa raundi ya awali utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Lwandamina aliiambia Nipashe jana kuwa wanataka kuutumia vyema uwanja wa nyumbani hivyo watacheza kwa tahadhari lakini ‘hawatapaki basi’ dhidi ya klabu hiyo kutoka Shelisheli.
“Tumewaona wapinzani wetu kupitia baadhi ya mikanda yao ya video, si timu mbaya, lakini lazima tuonyeshe kuwa tupo nyumbani, tutacheza soka la kushambulia lakini wakati huo huo tutakuwa makini kwenye kujilinda,” alisema Lwandamina.
Aliongeza kuwa anafahamu wapinzani wao watacheza soka la kujilinda kwa lengo la kuwabana ili wawe katika nafasi nzuri kwenye mchezo wa marudio utakaofanyika baada ya wiki mbili huko Shelisheli.
“Tutacheza kwa kasi zaidi dakika 15 za kwanza ili tupate bao la kuongoza, hii itatusaidia kushusha presha ya mchezo,” alisema.
Ajibu, Chirwa kuongozaKuelekea kwenye huo, Lwandamina, amepanga kuwatumia kwa pamoja washambuliaji, Ibrahim Ajibu na Obrey Chirwa.
Ajibu ambaye amekosa baadhi ya michezo ya ligi kuu kutokana na kuwa majeruhi lakini sasa amepona na leo ataongoza safu ya ushambuliaji pamoja na Chirwa ambaye kwa sasa yupo kwenye kiwango cha juu.
Aidha, golikipa namba moja, Youthe Rostand, naye anatarajiwa kuanza katika mchezo huo baada ya kupona na kufanya mazoezi ya pamoja na nyota wenzake.