YANGA kwa sasa watakuwa na uhakika wa kuwamaliza wapinzani wao, Township
Rollers ya Botswana katika mchezo wa hapa nyumbani baada ya Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF), kuwafutia mchezo wao dhidi ya Mtibwa Sugar.
Yanga watakutana na Wabotswana hao katika Ligi ya Mabingwa Afrika hatua
ya kwanza ambapo mchezo wa kwanza utapigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar,
Machi 6, mwaka huu.
Yanga ambao leo Jumatano watacheza na Ndanda FC, walipangwa kucheza na
Mtibwa Sugar ya Morogoro Machi 3, mwaka huu ambapo kwa sasa mchezo huo
umesogezwa mbele.
Katibu wa Yanga, Charles Mkwasa ameliambia Championi Jumatano, kuwa:
“Tuliiomba Bodi ya Ligi ya mchezo wetu na Mtibwa Sugar usogezwe mbele na
tayari tumepokea barua kutoka kwao ikionyesha kwamba mechi yetu hiyo
haitakuwepo kwenye tarehe hiyo. “Muda huu utakuwa sababu tosha kwetu
kujiandaa na kufanya vizuri katika mechi hiyo kwa sababu wachezaji
watakuwa na muda wa kutosha wa kupumzika,” alisema Mkwasa.