Jana (juzi) tarehe 9/2/2018 Bunge lilikuwa linajadili Taarifa ya mwaka ya Kamati ya Bunge ya Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje. Kutokana na muda kutokuwa wa kutosha, wabunge wachache walipata nafasi ya kuzungumza akiwemo Mbunge wa Mtama ndugu Nape Nnauye na Mbunge wa Iringa Mjini Mheshimiwa Peter Msigwa. Katika mazungumzo yake Nape alitaka Sheria ya usalama wa Taifa irekebishwe ili kuipa nguvu Chombo cha TISS kuzuia vitendo vya uhujumu uchumi badala ya hali ya sasa ambapo matukio mengi yanayohusu uhujumu uchumi hujulikana baada ya madhara kutokea. Mifano ya kashfa kubwa kama Richmond, EPA na Escrow ilitolewa. Mchungaji Msigwa alizungumzia kitendo cha kinyama dhidi ya Mbunge mwenzetu Tundu Lissu.
Waziri wa Usalama nchini Ndugu George Huruma Mkuchika alieleza kuwa TISS hawana shida na wanaweza kuendelea na kazi zao bila kuboreshwa. Siku hiyo nilipanga kuzungumza kuhusu masuala ya usalama wa Taifa hususan Kuhusu matukio ya kusikitisha ya Watu kupotea na hata jaribio la kumwua Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu. Sikubahatika kuzungumza ndani ya Bunge, kama nilivyosema sababu ya muda. Nina machache nilitaka kuyasema Bungeni na nimeona niyaandike. Mengine nitayasema kwa kina Bungeni siku za usoni Mungu akituweka hai. Haya machache ninayoandika ni kwa sababu ya kuonyesha kuwa sheria ya usalama wa Taifa inapaswa kufumuliwa na kuandikwa upya.
Sheria ya Usalama wa Taifa, sheria namba 15 ya mwaka 1996 ina mapungufu makubwa na pia inavunjwa vunjwa na chombo kinachoitekeleza. Pungufu la msingi ni kutokuwepo kwa sehemu ya ujasusi wa kiuchumi na hasa uchumi wa kimataifa Katika sheria nzima. Iwapo sheria ingekuwa ina vifungu vya kufanya ujasusi wa kiuchumi ingeweza kufunza watumishi wake masuala hayo na kulisaidia Sana Taifa kuepuka madhara mengi.
Kwa mfano, Hivi sasa Tanzania inapoteza fedha nyingi kwa sababu ya kushindwa kuleta ndege yake iliyoshikiliwa na watu wanaotudai huko Canada. Hili lisingewezekana iwapo TISS ingekuwa inafanya uchambuzi wa masuala hatari kwa Uchumi wetu. Ujasusi wa kiuchumi ungewezesha TISS kutambua uwezekano wa ndege zetu kushikiliwa na wangetoa mapendekezo ya namna ya kuokoa jambo hilo. TISS wangeweza kumshauri Rais namna bora kununua ndege ( kwa mfano badala ya kununua kutoka kiwanda cha Bombadier Canada wangenunua kutoka kiwanda cha Bombadier Ireland ambapo pengine hakuna wanaotudai). Hivi sasa ndege 2 zaidi za Tanzania zipo hatarini kushikwa ama zimeshikiliwa na Wananchi hatujaambiwa.
Kuna kampuni kutoka Japan inayoidai Serikali USD 65 milioni kwa kukiuka mkataba wa ujenzi wa barabara, imeshapata karatasi za mahakama huko Marekani ili kushika Boeing 787 Dreamliner inayonunuliwa na Tanzania. Pia kuna kampuni huko Uingereza inatudai USD 59 milioni tayari inanyemelea ndege ya Bombadier C300 inayoundwa huko Belfast Northen Ireland. Kampuni hiyo Ina karatasi za mahakama ya UK. Iwapo Sheria ya Usalama wa Taifa ingekuwa imetoa nguvu kwa TISS kufanya uchambuzi wa mambo kama haya ingeweza kuepusha nchi na changamoto hizi na nyengine nyingi. Mathalani, Hivi sasa kuna kashfa kubwa dhidi yetu kuhusu kuweka mawe kwenye korosho zetu tulizouza huko Vietnam. Kitengo cha Ujasusi wa kiuchumi kingeshachambua na kujua kama ni hujuma za mataifa mengine dhidi yetu au ni makosa ya wakulima wetu wenyewe. Ukiwahoji haya watu wa TISS, wanasema hawana mamlaka. Ni kweli, lazima sheria irekebishwe. Lakini kuna mambo TISS wanafanya wakiwa hawana mamlaka kisheria.
Kifungu cha 5(2) cha sheria ya usalama wa Taifa kinaizuia TISS kumfuatilia mtu yeyote wala kumpekua pekua au kumfanyia ujasusi kwa sababu ya msimamo wake kisiasa au Uhuru wake wa kuipinga Serikali. TISS inavunja sheria kila wakati kwenye eneo hili.
Nina mifano michache kuthibitisha hili. Mwaka 2017 aliyekuwa Waziri wa Habari Nape Nnauye alitishiwa bastola hadharani na watu wa usalama wa Taifa. Kabla ya hapo alikuwa anafuatiliwa na gari ambayo baadaye iligundulika ndio gari iliyokuwa inamfuatilia Tundu Lissu kabla ya kupigwa risasi zaidi ya 30. Mifano hii miwili ya Nape na Lissu inaonyesha kuwa TISS inafanya kazi kinyume cha sheria inayowakataza kufuata fuata watu wala kuwapekuapekua. TISS ilikuwa inamfuatilia Nape Nnauye na pia gari iliyokuwa inamfuatilia Tundu Lissu ilikuwa ya TISS kwani ilionekana kwenye matukio yote mawili.
Mambo haya hayawezi kufanyika bila IDHINI ya Mkurugenzi Mkuu wa Usalama na au Mkuu wa Uendeshaji wa Usalama wa Taifa. Kwa sasa nafasi hizi zinashikiliwa na Bwana Kipilimba na Bwana Robert Musalika, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa ambaye ni mzaliwa Geita na amekuwa Afisa Usalama wa Mkoa wa Tabora na baadaye mwakilishi wetu huko Addis Ababa Ethiopia. Bwana Kipilimba, ambaye sasa anamaliza muda wake ni mzaliwa wa Morogoro na amekuwa Benki Kuu na NIDA kabla ya kuwa Mkuu wa Usalama.
Hakuna tukio lolote la utekaji au mauaji linalofanywa na watu wa usalama bila IDHINI ya Mkurugenzi wa Operesheni ambaye sasa ni Robert Musalika. Likitokea tukio la namna hiyo bila idhini ya Director of Operations basi ni lazima yeye atumie sheria kufanya uchunguzi na kupendekeza hatua za kuchukua.
Sheria ya usalama wa Taifa kifungu cha 14 kinatoa mamlaka kwa TISS kuchunguza jambo lolote linalookena ni tishio kwa nchi. Kifungu hiki kimeliweka jukumu hili kama WAJIBU wa chombo hiki ( duty to investigate) hivyo majibu mepesi kuwa sio kazi ya TISS kuchunguza hayana msingi kabisa.
Kuna matukio ambayo ni tishio kwa usalama wa Wananchi ambayo mpaka sasa hakuna majibu ya Serikali. Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi Bwana Azory Gwanda amepotea sasa zimefika siku 85 hivi na hakuna majibu yeyote ya Serikali. Azory alikuwa anaandika Habari za kiuchunguzi kuhusu masuala ya Kibiti na kuokotwa kwa miili ya Wananchi kwenye fukwe zetu. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Kibondo Bwana Simon Kanguye alitekwa na maafisa usalama wa Taifa mjini Kibondo siku moja kabla ya ziara ya Rais wa Tanzania mkoani Kigoma na mpaka leo hajulikani alipo. Matukio haya matatu ya Watu kupotea na miili kuokotwa ni matukio yanayolazimisha TISS kuyachunguza kwa kutumia kifungu cha 14 cha sheria yake ya mwaka 1996.
Kwa kuwa hawangaiki nayo ni rahisi kutafsiri kuwa kuwa TISS chini ya Mkurugenzi wa Uendeshaji Bwana Musalika wameidhinisha haya. Ni vema ifahamike kuwa kabla ya kurudi nyumbani Bwana Musalika alikuwa Mfanyakazi wa Ubalozi wetu Addis Ababa, Ethiopia nchi ambayo rekodi yake ya Watu kupotea, kutekwa, kufungwa na hata kuuwawa inatia fora. Bwana Musalika anapaswa kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Usalama ili ajieleze ni kwanini asiwajibishwe kwa kushindwa kutimiza wajibu wake wa kifungu cha 14 cha sheria ya usalama wa Taifa.
Nimetaja hapo juu suala la Mbunge Tundu Lissu. Jana Kamati Ulinzi, Usalama na Mambo ya Nje ya Mheshimiwa Adadi Rajabu ilionyesha kusikitishwa na tukio la Tundu kupigwa risasi na kupendekeza kuwa wabunge wapewe Ulinzi. Ni vema ieleweke kuwa mahala anapoishi Mbunge akiwa Dodoma kwenye mkutano wa Bunge ni eneo la Bungeni ( precincts of parliament). Kifungu cha 2 cha sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ( sheria namba 3 ya mwaka 1988 ) kimetafsiri kuwa eneo la Bunge ni pamoja na malazi ya Mbunge. Kwa hiyo Tundu Lissu alipigwa Risasi Katika eneo la Bunge kisheria ambalo linapaswa kulindwa na vyombo vya Serikali.
Katika mantiki ya kawaida kabisa tukio la namna hiyo haliwezi kufanyika bila idhini ya chombo kinachoshughulika na usalama na kwa maana hiyo Mkurugenzi wa Operations wa TISS. Nilisikitishwa Sana na kitendo cha Kamati ya Ulinzi na Usalama kusikitishwa tu na tukio la Kinyama dhidi ya Tundu Lissu, Kamati ilipaswa kwenda mbele na kumwajibisha Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa na Naibu wake ambaye anasimamia Operations. Kamati haikupaswa kuomba tu wabunge kupatiwa Ulinzi, bali ilipaswa kuhoji ni kwanini sheria ya Haki na Kinga za wabunge haitekelezwi na vyombo vya ulinzi na usalama.
Tunaweza kujadili mambo haya sasa hivi kwa sababu Tundu Lissu yupo kitandani Katika hospitali nchini Ubelgiji ama Ben Saanane, Azory Gwanga na Simon Kangoye wamepotezwa. Kama tusipochukua hatua mahususi na madhubuti za kuifumua TISS na kuiunda upya, watu wengi zaidi watapotea, kupigwa risasi na kuokotwa kwenye fukwe zetu. Sijui tunasubiri nini kitokee mpaka tukubali ukweli kuwa TISS inapaswa kufumuliwa na Viongozi wake wa sasa wanapaswa kuwajibishwa na kufikishwa kwenye mahakama kujibu mashtaka ya mauaji na kupoteza watu.
Vile vile kama hatutachukua hatua kuunda kitengo madhubuti cha ujasusi wa kiuchumi kwa mujibu wa sheria tutaendelea kupigwa tu kwenye mikataba ya kimataifa na kuathirika sana kiuchumi kama Taifa. Huu ni wakati mwafaka kabisa kuifumua TISS na kuiunda upya ili itumikie nchi yetu na kuhakikisha usalama wa Wananchi na usalama wa Uchumi wa Taifa. #ReformTISSnow