Gazeti la City Press limefahamishwa pasi na shaka kwamba wanasheria watano waandamizi walipendekeza kwa ujumla wao Ijumaa iliyopita kwamba Zuma afikishwe mahakamani na ashtakiwe kwa mashtaka ambayo yaliondolewa awali.
Inaaminika walitiliana saini makubaliano ya awali ambayo Ijumaa alikabidhiwa Mkurugenzi wa Taifa wa Mashtaka Shaun Abrahams, wakimtaarifu kuhusu mapendekezo yao.
Kwa hali hiyo, Zuma anatarajiwa kukabiliwa na mashtaka 18 ya ufisadi, utakatishaji fedha na udanganyifu yote yakitokana na malipo yenye utata 783 aliyopokea siku za nyuma.
Huu unaweza kuwa mwanzo wa mapambano kadhaa ya kisheria dhidi ya Zuma ambaye hivi karibuni alilazimishwa na chama chake cha ANC kujiuzulu. Anatarajiwa kuwa mlengwa mkuu wa tume inayochunguza kashfa ya serikali kuwekwa mfukoni na mafisadi.
Tangu Jumatano wiki iliyopita, timu ya waendesha mashtaka imekuwa ikifanya kazi kuweka pamoja mashtaka yanayoelezea makosa ambayo Zuma na mshtakiwa mwingine watakabiliwa nayo baada ya miaka mingi ya ushindani wa kisheria.
Vyanzo kutoka ndani ya vyombo vya usalama zinasema ingawa kulikuwa na kutofautiana kwingi na mvutano juu ya nani anapaswa kubaki kuwa sehemu ya timu ambayo inaweza kumshtaki Zuma, wote walikubaliana kwamba alishindwa kutoa hoja ya kushinikiza mashtaka yake yatupwe.
"Hakuna kurudi nyuma. Zuma anapaswa kushtakiwa kortini. Siwezi kufikiri kama Abrahams anaweza kupuuza mapendekezo ya waendesha mashtaka watano aliowateua kumwongoza juu ya uamuzi huu," alisema mtoa habari.
"Kwa kweli, bosi wa mashtaka wa KwaZulu-Natal Moipone Noko alisisitiza Desemba kuwa Zuma lazima afikishwe mahakamani siku 14 baada ya korti kutoa uamuzi wa kutupilia mbali mashtaka hayo kwamba hayana maana.”