Abiria Adaiwa Kumnyonga Kondakta wa Daladala Hadi Kufa

DAR ES SALAAM: Kondakta wa daladala aina ya Nissan Civilian lenye namba za usajili T 247 DDT lililokuwa likifanya safari zake kati ya Temeke, Dar na Vikindu, Pwani, Abdallah Kikoto (36), anadaiwa kunyongwa na abiria wake hadi kufa, Ijumaa Wikienda linaripoti habari hii mbaya.

Taarifa zilizolifikia Ijumaa Wikienda zilieleza kuwa, katika tukio hilo lililojiri mwishoni mwa wiki iliyopita, abiria huyo alipanda basi hilo wakati likitokea maeneo ya Chamazi ambako linalazwa baada ya kazi. Ilielezwa kuwa, chanzo cha yote hayo ni mgogoro wa kurudisha chenji.

KISA NA MKASA

Akisimulia kisa hicho, dereva aliyekuwa akiendesha daladala hilo, Haji Kitara alisema kuwa, ilikuwa majira ya asubuhi, yeye na kondakta wake walikwenda Chamazi kuchukua daladala hilo na kuanza kazi ambapo wakiwa njiani kuelekea kwenye ‘ruti’ yao walianza kupakia abiria.

Aliendelea kusema: “Tulipofika njiani, nilianza kusikia kondakta wangu na huyo abiria wakilumbana. Huyo abiria alikuwa akisema kuwa ametoa noti ya shilingi elfu moja hivyo anataka arudishiwe chenji yake shilingi mia sita huku kondakta wangu yeye akisema tayari alishamrudishia.

“Waliendelea kulumbana hadi tulipofika Tandika-Msikiti wa Wapemba, Temeke, yule abiria alishuka na kumpora kondakta pesa zote alizokuwa nazo ili kufidia chenji yake.


Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, (ACP) Emannuel Lukul.

KABARI YA HATARI

“Hapo ndipo mzozo ulikolea maana kondakta naye hakukubali kuporwa pesa zote kwa ajili ya hiyo mia sita. Nilipoona vurugu imekuwa kubwa, nilikimbiza basi hadi Kituo Kidogo cha Polisi cha Tandika, wakati huo yule abiria alikuwa amemkaba kondakta wangu kabari moja ya hatari sana.

“Tulipofika kituo cha polisi yule jamaa alimuachia konda kwa muda, wakati huo alikuwa ameshamchania suti yake ya juu na kumbakiza na ‘singlendi’, lakini wakiwa hapo kituoni waliendelea kubishana ndipo yule abiria akamvaa tena kondakta na kumnyonga kwa singlendi aliyobaki nayo.

“Yule abiria alimng’ang’ania kondakta huku akimnyonga na singlendi aliyovaa ndipo polisi waliokuwa kituoni hapo wakaingilia kati na kumnasua kondakta huyo akiwa amekabwa, lakini abiria huyo aliendelea kufanya hivyo hali iliyosababisha askari watumie rungu kumpiga nalo mikononi ndipo alipomuachia.

“Baada ya kumuachia kondakta huyo alianguka hapohapo na kupoteza fahamu hivyo polisi wa Kituo cha Tandika waliwasiliana na wenzao wa Kituo cha Chang’ombe ambao walipofika walituchukua wote na kutuhamishia Chang’ombe huku kondakta akiwa hajitambui.


AMEKATA ROHO

“Tulipofika Kituo cha Chang’ombe, askari wa pale walipomuona kondakta akiwa hajitambui walipatwa na shaka, wakamdhibiti huyo abiria na kumuwahisha Hospitali ya Temeke.

“Tukiwa pale hospitalini, daktari aliyempokea alituambia tayari kondakta huyo alikuwa ameshakata roho muda mrefu na alipoufanyia uchunguzi mwili wake, alisema kilichomuua ni kukosa pumzi.”

KAKA WA MAREHEMU

Kufuatia tukio hilo, mwandishi wetu alifika nyumbani kwa wazazi wa marehemu huyo, Mtoni-Mtongani Mtaa wa Wandengereko jijini Dar na kuzungumza na kaka wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Musa Kikoto ambaye alisema kuwa, alizipokea taarifa hizo kwa simanzi kubwa kwani kufuatia kifo hicho, mdogo wake huyo alikuwa ameacha mke na watoto wanne.

“Unajua mzazi unapokuwepo ndiyo unakuwa na jukumu la kupambana na malezi ya familia yako na usipokuwepo mambo ni vigumu kwenda inavyotakiwa, sasa mdogo wangu ameondoka mapema na kutuachia majukumu mazito ya kuwalea na kuwasomesha watoto wote hao ambayo bado tunayatafakari,” alisema kaka huyo.

Musa alisema kuwa, mdogo wake alizikwa katika Kijiji cha Mtawanya wilayani Kibiti mkoani Pwani.

KAMANDA TEMEKE

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi, (ACP) Emannuel Lukula alithibitisha kutokea tukio hilo na kusema mtuhumiwa anashikiliwa kwa tuhuma za mauaji.

“Ni kweli kulitokea tukio hilo ila si kwamba kondakta huyo amefia kituo cha polisi kwa kuwa daktari amethibitisha kifo ila hatuwezi kujua kama amefia njiani wakati akipelekwa hospitali au vinginevyo.

“Huyo jamaa (mtuhumiwa) tayari yuko mbaroni akikabiliwa na kesi ya mauaji, hata hivyo ndugu mwandishi sasa hivi sipo ofisini ningekuwepo ningekupa data nyingi zaidi za tukio hilo ikiwemo jina la mtuhumiwa na mengineyo,” alimalizia Kamanda Lukula.



STORI: Richard Bukos, IJUMAA WIKIENDA
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad