Chama cha ACT Wazalendo kimekabidhi mifuko 40 ya Saruji kama mwendelezo wa utekelezaji wa ahadi ya kujenga Zahanati kwenye Kijiji cha Chidolu kilichopo Wilaya ya Bahi Mkoa wa Dodoma ambacho kinaongozwa na ACT Wazalendo.
Ahadi ya kujenga zahanati hiyo ilitolewa na Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Ndugu Zitto Kabwe.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mifuko hiyo ya Saruji, Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT Wazalendo Ado Shaibu amesema kwamba chama cha ACT kinaamini kuwa mbali na kuikosoa serikali pia wanawajibu wa kushirikiana na wananchi katika kufanya maendeleo.
"Sisi ACT Wazalendo tunaamini kwa dhati kuwa mbali na kutekeleza wajibu wa kuikosoa serikali, tunao pia wajibu wa kushirikiana na wananchi katika kujiletea maendeleo. Kazi ya upinzani haiwezi kuwa kupiga mdomo pekee. Itakuwa ni faraja iwapo Kijiji hiki ambacho hakina Zahanati tangu uhuru kitapata Zahanati katika Uongozi wa ACT Wazalendo" Ndg. Shaibu.
Ameongeza "Nipo hapa kumuwakilisha Kiongozi wa Chama Ndugu Zitto Kabwe ambaye aliahidi kushirikiana na nyinyi kuhakikisha Kijiji hiki ambacho kinaongozwa na ACT Wazalendo kinapata Zahanati ya Kijiji. Yeye yupo kwenye ziara ya kuzitembelea Kata zinazoongozwa na ACT Wazalendo".
Mbali na hayo Kiongozi huyo wa ACT Wazalendo amewapongeza wananchi wa Chidolu kwa kujitolea kuchimba msingi wa Zahanati na kufyatua matofali na kuwakumbusha kwamba maendeleo ya kweli hayawezi kushushwa kutoka juu bali lazima wananchi nao washiriki kikamilifu kwenye programu za maendeleo.
ACT Wazalendo Watelekeza Ahadi Yake Sasa Kujenga Zahanati Dodoma
0
March 01, 2018
Tags