Afande sele ametoa kauli hiyo kupitia ukurasa wake wa kijamii jioni ya leo ikiwa zimepita takribani siku nne tokea alipotangaza nia ya kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) mbele ya Rais Dkt. Magufuli aliyekuwepo katika ziara ya kikazi Mkoani Morogoro kwa lengo la kuunga mkono jitihada zake anazozifanya katika kupigania na kukiomba chama kimpokee kama kijana wao.
"Ninachofahamu ni kwamba katika hatua zote nilizopitia ndani ya ulimwengu wa kisiasa sikua navunja sheria za nchi wala kumdhuru mtu yeyote zaidi ya ukweli kwamba nilikua natimiza haki zangu za kikatiba na kidemokrasia kama raia mwema wa nchi huru na ya kidemokrasia", amesema Afande Sele.
Aidha, Afande Sele amesema kipindi chote alichokuwa nje ya ulingo wa siasa alikuwa anapokea simu za viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani wakiwa wanamtaka ajiunge na vyama vyao kwa lengo la kuwaongezea nguvu katika kudai haki za kikatiba kwenye mkoa huo.
"Kilicho nifadhahisha ni kuona wale rafiki zangu waliokua wananitaka nijiunge na vyama wapendavyo wao kwa madai ya mimi kutimiza haki zangu za kikatiba na kidemokrasia ili tukapingane na chama tawala cha CCM walichodai kuwa kinawabana watu katika kutimiza haki zao muhimu za kikatiba, wakawa wananipigia simu tena kulaani, kulaumu na kupinga uamuzi wangu huo muhimu na halali wa kikatiba na kidemokrasia waliokua wananiomba kila siku nijiunge upande wao ili tukaupiganie", amesema Afande Sele.
Pamoja na hayo, Afande Sele ameendelea kwa kusema "wanapinga mimi kufanya maamuzi yangu ya kutimiza haki yangu ya kikatiba na wakati huo wanataka mimi nijiunge nao kwenda kuandamana kudai haki hizo ambazo nao wanadai zimebanwa na CCM. Hakika marafiki hawa wamenipa somo jipya la kujua namna vijana wengi wa kitanzania tunavyofanya matumizi mabaya ya vichwa vyetu katika kufikiri na kuchanganua mambo, kwamba wanapinga mimi kutimiza haki zangu za kikatiba na kidemokrasia wakiwa hawajashika dola je kesho wakishika dola watamtendeaje yule anaetenda kinyume na watakavyo wao?".
Kwa upande mwingine, Afande Sele amesema ni kweli amehamia CCM kama walivyomuona akijitangaza kwani ameweza kutimiza haki yake ya kidemokrasia na kikatiba kama walivyokuwa wanaidai wao kutoka ndani ya chama tawala na serikali yake kiujumla.