Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imeuagiza upande wa Jamhuri kukamilisha kwa haraka upelelezi wa kesi ya vigogo watatu wa Shirikisho la Soka (TFF), akiwamo aliyekuwa rais Jamal Malinzi, ili haki iweze kutendeka kwa pande zote mbili. Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.
Hakimu Mashauri alisema ni aibu kila tarehe ya kesi inapopangwa upande wa Jamhuri kudai upelelezi bado haujakamilika huku washtakiwa wakiwa mahabusu zaidi ya miezi tisa sasa.
"Washtakiwa wako mahabusu miezi tisa sasa imepita bila ya upelelezi kukamilika, upande wa Jamhuri kamilisheni upelelezi haraka ili pande zote mbili ziweze kupata haki," aliagiza Hakimu Mashauri.
"Mahakama yangu inatupilia mbali (hata hivyo) maombi ya utetezi ya kwamba ina mamlaka ya kuwaachia (huru) washtakiwa chini ya kifungu cha 225 kidogo cha (5) cha sheria ya Mwendo wa Makosa ya Jinai (CPA)."
Akifafanua uamuzi wake huo, hakimu huyo alisema mahakama hiyo kisheria haina mamlaka ya kuwaachia washtakiwa hao kwa sababu miongoni mwa mashtaka yanayowakabili ni ya kughushi ambayo hayaingii katika kanuni ya kukamilisha upelelezi ndani ya siku 60.
Mbali na Malinzi (58), washtakiwa wengine ni aliyekua Katibu Mkuu, Mwesigwa Selestine(47) na Mhasibu, Nsiande Mwanga (28) wote wa TFF.
Wakati huo huo, wakili wa utetezi Kashindye Thabiti alidai mahakamani hapo kuwa hukosa ruhusa ya kuzungumza na washtakiwa wanapokwenda mahabusu ya Magereza.
"Mheshimiwa tunaomba mahakama yako itusaidie kupata kibali cha kuwaona washtakiwa kwa sababu wateja wetu wana haki ya kuongea na mawakili ili kuwapa mwongozo dhidi ya kesi yao," alidai Thabiti.
Wakili wa serikali, Upendo Temu alijibu hoja ya utetezi kwa maelezo ufuate utaratibu uliowekwa na Jeshi la Magereza wa kuwaona washtakiwa walioko mahabusu.
Hakimu Mashauri alisema katika kutembelea mahabusu waliopo magereza ni lazima utaratibu uliowekwa na jeshi hilo ufuatwe. Alisema kesi hiyo itatajwa Machi 28.
Machi 8, mwaka huu upande wa utetezi ulilalamika mahakamani hapo kuwa kesi hiyo imechukua muda mrefu tangu washitakiwa walipofikishwa kwa mara ya kwanza Juni, mwaka jana.
Malinzi na wenzake walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Juni 29 wakikabiliwa na mashtaka 28 ikiwamo ya kughushi na kutakatisha fedha dola za Marekani 375,418.