Askari Polisi wa Kituo Kidogo cha Lukula katika Kata ya Kitunda wilayani Sikonge, Jebasa Charles amekamatwa na jeshi hilo akituhumiwa kukutwa na mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kiwele akifanya mapenzi kituoni hapo.
Akizungumza na waandishi wa habari Machi 15, mwaka huu, Diwani wa Kata ya Kitunda wilayani Sikonge mkoani Tabora, Mbwana Seif alisema askari huyo walimfanyia mtego na mzazi wa mwanafunzi Farida Juma kituoni hapo kwa muda wa siku tatu na kufanikiwa kumkamata.
Seif alisema tukio hilo lilitokea saa 11 alfajiri wakati askari huyo alipofungua mlango ili kumtoa mwanafunzi huyo wa kidato cha pili, ndipo akakutana na wananchi na mzazi wakiwa mlangoni kisha kuwakamata wawili hao.
Aidha, diwani huyo alidai taratibu zilifanyika za kumpeleka mwanafunzi huyo hospitalini kupata vipimo, ambako walidai ni mjamzito. Hata hivyo, Seif alisema baada ya kukamatwa kwa askari huyo na kumweka ndani, mzazi hakuridhika na aliomba kituoni hapo aondolewe na kupelekwe Kituo cha Polisi Wilaya ya Sikonge. Diwani huyo alisema wananchi wa Kata ya Kitunda wamekasirishwa Kituo Kidogo cha Polisi Lukula kugeuzwa nyumba ya kufanyia maasi.
Babu wa mwanafunzi huyo, Juma Kaseka ambaye ndiye aliyekuwa anaishi na binti huyo alisema kama hatua hazitachukuliwa ipasavyo na Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Wilbroad Mutafungwa hawatosita kumtafuta Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro ili awasaidie. Kaseka alisema Machi 13, mwaka huu saa 4 usiku, mwanafunzi aliondoka nyumbani baada ya kupata chakula na hakujulikana alipokwenda.
Alisema majirani waliwaambia walimuona Kituo Kidogo cha Lukula na walitoa taarifa kwa uongozi wa kijiji akiwemo mtendaji na mwenyekiti wa kijiji hicho na kuchukua hatua hiyo ya kumvizia na kumkamata. Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Wilbroad Mutafungwa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kueleza kuwa ni mwanafunzi wa shule hiyo wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Kiwele. Kamanda alisema askari huyo amekamatwa jana na kufikishwa Kituo Kikuu cha Wilaya ya Sikonge kwa ajili ya kuhojiwa na wanatarajia kumuhoji mwanafunzi huyo na kumfanyia vipimo ili kuthibitisha madai yake.