Askofu Mkuu KKKT :Hatukubali Kuzibwa Mdomo na Kiongozi Yeyote wa Kisiasa au Serikali

Askofu Mkuu KKKT :Hatukubali Kuzibwa Mdomo na Kiongozi Yeyote wa Kisiasa au Serikali
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo ameonya kwamba asitokee kiongozi yeyote nchini wa kisiasa au serikali ambaye atajaribu kuwazuia na kuwaziba midomo viongozi wa dini kutekeleza wajibu wao wa kukemea na kuonya juu ya maovu yanayoendelea hapa nchini.

Dk. Shoo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, pia amesema kamwe kanisa halitanyamaza kimya kwa wanasiasa wenye tabia ya kutumia nafasi zao kuligawa taifa vipande vipande.

Alizungumza hayo  jana kwenye ibada maalumu ya kusataafu kwa aliyekuwa Mchungaji wa Usharika wa Masama Kati, John Mshau wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro.

“Wajibu wa viongozi wa dini ni kuonya na kukemea yale mabaya yanayoendelea nchini na si vinginevyo na kwamba  asijaribu kutokea mtu yeyote kuwazuia viongozi wa dini kufanya wajibu huo kwani ni sawa na kupingana na Mungu.

“Wajibu wetu ni kuonya, kushauri, kukemea na tunatenda hivyo, asijaribu kuja mtu yeyote kutuzuia kufanya hivyo kwani neno la Mungu linasema bwana hutegemeza wenye upole na huangusha chini wenye hila, hivyo sisi kama viongozi wa dini hatutakubali kunyamaza tutasema na kukemea maovu,” amesema

Pamoja na mambo mengine, Dk. Shoo aliwaonya viongozi wote wa kisiasa nchini kuacha kutumia vyama vyao kuligawa taifa na kwamba suala hilo halitaweza kuvumiliwa na viongozi wa dini na wataendelea kusema na kuonya.

Akitolea ufafanuzi waraka ulioandaliwa na Baraza la Maaskofu 27 wa KKKT, Machi 15 Jijini Arusha alisema walifunga na kuomba Mungu kwa lengo la kupata ujumbe sahihi ili wautoe kwa waumini wa kanisa hilo na Taifa kwa ujumla na kwamba hawakukurupuka kutoa ujumbe huo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad