Wanamuziki maarufu wa muziki wa dansi, Nguza Viking, maarufu kwa jina la “Babu Seya” na mwanaye, Johnson Nguza au “Papii Kocha” leo Machi 9, 2018 wameeleza shughuli mbalimbali walizokuwa wakifanya gerezani.
Wakati Papii Kocha akisema alikuwa akijishughulisha na ushonaji wa mazulia, Nguza amesema alichaguliwa kuwa mnyampala, akiwa na jukumu la kusimamia wafungwa katika masuala mbalimbali.
Babu Seya, ambaye ni mtunzi wa kibao maarufu cha “Seya”, na mwanae Papii Kocha ambaye wameshirikiana katika wimbo huo, ni miongoni mwa wafungwa 8,157 waliosamehewa na Rais John Magufuli siku ya Uhuru wa Tanganyika.
Walikuwa kati ya wafungwa 61 waliokuwa na adhabu za vifungo vya maisha na kunyongwa ambazo si rahisi kupata msamaha wa kawaida wa mkuu wa nchi unaotolewa siku ya sherehe hizo.
Wakihojiwa leo Ijumaa Machi 9, 2018 katika kipindi cha Leo Tena kinachorushwa na Redio Clouds, Papii Kocha amesema wakati akiwa gerezani alikuwa akifanya shughuli za ushonaji wa mazulia pamoja na vikapu.
“Nilikuwa sijui kabla ya kwenda gerezani lakini tulijifunza na kwa sasa naweza vizuri,” amesema.
Amesema mbali na ushonaji, pamoja na baba yake walikuwa wakifanya mazoezi ya muziki mara tatu kwa wiki.
Wa upande wake Nguza amesema alivyokuwa gerezani alikuwa nyampala mkuu wa gereza baada ya kuteuliwa na uongozi wa Jeshi la Magereza.
“Ni busara tu zilinifanya nikateuliwa. Kazi ilikuwa ngumu na isitoshe unaowaongoza ni wahalifu lakini busara tu ilitumika,” amesema.