Baraza la Maaskofu Lakomalia Katiba Mpya

Baraza la Maaskofu Lakomalia Katiba Mpya
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limesema ili amani iendelee kuwepo majadiliano ndio nyenzo kuu itakayosaidia kuhuisha mchakato wa Katiba Mpya.

Pia limeitaka Serikali kuweka nia ya dhati na kutii kiu ya Watanzania iwapo wengi wao watahitaji mchakato wa Katiba Mpya uendelezwe.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa TEC, Padri Daniel Dulle, wakati akifungua kongamano la kujadili Katiba na ujenzi wa amani wakati wa uchaguzi lililoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Hii ni mara ya pili katika kipindi kisichopungua mwezi mmoja kwa TEC kutoa kauli kama hiyo, kwani kumbukumbu zinaonyesha kuwa Februari 11 mwaka huu, Baraza hilo katika ujumbe wake wa Kwaresma lilitoa msimamo katika masuala matatu kisiasa, kiuchumi na kijamii ambapo lilionya kutozingatia matakwa ya Katiba katika kuendeleza shughuli za kisiasa.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Padri Raymond Saba, Padri Dulle, alisema baada ya mchakato wa Katiba Mpya kukwama sasa ni fursa nzuri ya kuendeleza mchakato huo kwa njia ya majadiliano ili kudumisha amani.

“Majadiliano ni nyenzo ya kupambana na tabia ya ubinafsi, ili kujenga umoja huo lazima kuwepo na upendo, mshikamano na maridhiano ya watu na kila mtu kupewa nafasi ya kutoa maoni hata kama yanapingana na mtu mwingine na ukiwa unapatanisha kwa njia hiyo unaitwa mwana wa Mungu.

“Ndilo lengo la kukaa hapa na kujadiliana ili kujenga Taifa letu kwa lengo la kupata Katiba Mpya ambayo kila mmoja anaitamani. Kunapotokea mtafaruku ndipo kunakuwa na chuki kama kikundi kingine hakishirikishwi.  Haki na amani ni matunda tu, kwani ukosefu wa haki ni chanzo cha vita inayoacha makovu na chuki za kisiasa kwenye chaguzi. Kama tunataka kukwepa haya makovu lazima watu tujenge tabia ya kujadiliana,” alisema.

Alisema tangu miaka ya 1800, Kanisa Katoliki limekuwa likitoa miongozo kuhusu masuala ya utawala ili kudumisha amani.

“Suala la Katiba ni nia ya watu wote si ya mtu mmoja, ni sauti ya watu na kadiri watu wanavyohitaji sheria na miongozo. Pengine kikundi kikubwa kinahitaji kidogo hakihitaji cha msingi ni kuangalia wananchi wanahitaji nini kwani kwa mujibu wa ibara ya nane ya Katiba ya sasa, Katiba ni mali ya wananchi,” alisema.

Aidha, akichangia mjadala katika kongamano hilo, Profesa Mwesiga Baregu ambaye alikuwa akimwakilisha Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia nchini (TCD), James Mbatia, alionya Serikali kuhakikisha kabla ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2020, Katiba Mpya inapatikana.

Baregu ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema ni vema kukamilisha kiporo hicho cha Katiba kwa sababu viashiria vyote vya hatari vimekwishaonekana katika chaguzi ndogo zilizofanyika hivi karibuni hususani Jimbo la Kinondoni.

“Tujitahidi kwa vyovyote vile kuhakikisha uchaguzi unaokuja si tu wa haki lakini matokeo yake yawe ya kuaminika. Kwa sababu inaelekea chaguzi zetu kuwa ‘security election’.

“Uchaguzi uliopita Kinondoni tunaambiwa kuna vituo ambavyo polisi walizidi wapiga kura, huu uwapo wa polisi kwenye chaguzi ni tatizo kwa sababu inatafsirika kuwa lazima kutakuwa na machafuko au kuna kitu polisi wamegundua,” alisema.

Aidha, Profesa Baregu, alipendekeza njia tatu za kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya kwa kuwa hali iliyopo lazima kuwepo na njia ya kuishawishi Serikali.

“Kwanza twende kwenye kura ya maoni, tunaweza kutangaza kura ya maoni kuhusu Katiba pendekezwa ila sijui kura ya maoni kama itaendeshwa kwa uhuru au haki. Kwa sababu hata katika Katiba pendekezwa tumeona asilimia 85 ya maoni ya wananchi yamenyofolewa.

“Pili kuundwe Bunge la Katiba lenye wajumbe wasiokuwa wabunge kwani hawa waliopo bungeni watatengeneza Katiba ya kuwalinda na tatu kuundwe tume ya wataalamu wa Katiba kama walivyofanya wenzetu Kenya, kwani mahali tulipofika lazima tutoke kwenye ujumla ujumla tuwe na mashinikizo ya kuitaka Serikali ifanye nini kabla ya uchaguzi mkuu ujao,” alisema.

Pamoja na mambo mengine alieleza kushangazwa na baadhi ya mawaziri wanaodai kuwa rasimu ya pili ya Katiba Mpya iliwalisha wananchi maoni jambo ambalo si kweli.

“Baadhi ya mawaziri wanasema mambo ya kipumbavu eti watu wamelishwa maneno na tume, kusema kweli hiyo ni dharau kwa watu kuwa hawawezi kusema Rais apunguziwe madaraka na mambo mengine,” alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha ACT – Wazalendo, Yeremia Maganja, alisema hitaji la Katiba ni tangu vizazi na vizazi hivyo Serikali haitakiwi kupuuza takwa la wananchi.

“Pia tunaona tatizo linaloikabili nchi yetu ni taasisi ya rais kutokuwa na mamlaka inayoisimamia, ndiyo maana rais anaonekana kuwa amegeuka Mungu mtu,” alisema.

Aidha, Rais mstaafu wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), John Seka, alisema ili kuwepo na chaguzi za kidemokrasia lazima kuwepo na mfumo wa kisheria unaozingatia kutibu vidonda vya chaguzi zilizopita.

“Pia kuwe na miundombinu wezeshi kwa vyama vyote ikiwamo kupatiwa gharama za uchaguzi pamoja na mambo mengine,” alisema.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Zanzibar, Musa Kombo Musa, alilaumu baadhi ya Wazanzibari walioshiriki kupitisha Katiba pendekezwa na kudai kuwa hao ndio wamesababisha mchakato huo wa Katiba Mpya usitimie.

“Sijui Wazanzibari waliokuwa kwenye bunge lile waliingiwa na wazimu gani, wamesababisha tuendelee kukandamizwa na Tanzania Bara. Wazanzibari tumechoka na mambo tunayofanyiwa, tunahitaji Katiba ya Jaji Warioba,” alisema.

Naye Mwakilishi wa Asasi za kiraia, Deo Bwire, alitoa wito kwa Rais John Magufuli, kukutana na makundi mbalimbali ikiwamo viongozi wa dini na wa kisiasa kama alivyokuwa akifanya mtangulizi wake Rais Jakaya Kikwete, ili kufufua mchakato wa Katiba Mpya.

Akifunga kongamano hilo, Kaimu Mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga, alisema uhitaji wa Katiba Mpya hujitokeza kila mara baada ya chaguzi kufanyika.

Alisema ili kuzuia matukio ya uvunjifu wa amani, ni vema Serikali ikahuisha mchakato wa Katiba Mpya kabla ya kuelekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2020.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Sio mbaya Maaskofu kudai katiba mpya ila madai yao yapo kisiasa zaidi kuliko kiutumishi wa Mungu. Yule Padre feki au sijui akijiita mtume Tito aliendesha mahubiri feki na kama si kwa nguvu za wananchi na serikali mpaka leo angekuwa yupo mitaani anahubiri. Au kumdhibiti Tito na mahubiri yake feki umoja wa Maaskofu ulihitaji katiba mpya pia?

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad