Binti mmoja wa Kipalestina aliyekamatwa baada ya kumchapa kofi mwanajeshi wa Israel amekiri kosa na atatumikia kifungo cha miezi minane gerezani kufuatia maafikiano kati yake na upande wa mashtaka.
Msichana huyo Ahed Tamimi alikiri kuwa na hatia kwa makosa manne aliyokuwa akishtakiwa kati ya 12 yaliyokuwa yakimkabili, ikiwemo shambulio la mwili, wakili wake ameeleza.
Kadhalika, atalipa faini ya shekeli 5,000 sawa na dola 1,440 .
Binti huyo mwenye miaka 17 alikamatwa baada ya kunaswa kwenye picha ya video akiwakabili wanajeshi wawili nje ya nyumba yake mwezi Desemba.
Uamuzi wa mahakama unamaanisha kuwa ataachiwa huru kipindi cha majira ya joto kwa sababu hukumu yake imehesabu siku alizokaa korokoroni, mwanasheria wake Gaby Lasky amenukuliwa na shirika la habari la AFP.
Kwa Wapalestina, Ahed Tamimi, ambaye kwa kipindi hicho alikuwa na miaka 16 wakati tukio lilipotokea Ukingo wa Magharibi, ni ishara ya kutounga mkono makazi ya Israeli.
Lakini waisraeli wanamuona kama mtu mwenye vurugu na kutafuta umaarufu.
Kesi yake ilikuwa ya ndani kwenye mahakama ya kijeshi katika eneo la ukingo wa magharibi tarehe 13 Februari.
Mwanasheria wake alitaka mashtaka hayo yasomwe hadharani lakini Jaji aliamua kesi hiyo iendelee huku ikirekodiwa kwenye kamera.
Ahmed Tamimi alipigwa picha ya video na Mama yake,Nariman, alipokuwa akigombana na wanajeshi wenye silaha, katika kijiji cha Nabi Saleh tarehe 15 mwezi Desemba, baada ya kutokea maandamano yaliyokuwa yakipinga hatua ya Marekani kuutambua mji wa Jerusalemu kuwa mji mkuu wa Israel.
Tukio hilo lililorekodiwa lilikuwa kwenye ukurasa wa Faceook wa Nariman na video ya ugomvi huo ilisambaa sana.Katika video hiyo,Ahed Tamimi alionekana akimpiga teke mwanajeshi mmoja na kumchapa kofi la usoni, na kumtishia kumpiga mwanajeshi mwingine.
Ahed alikamatwa majira ya usiku na kukabiliwa na shutuma 12, kushambulia, kuchochea, kuingilia kazi za wanajeshi na kurusha mawe.
Mama yake pia alishtakiwa kwa makosa ya kufanya uchochezi kwenye mtandao wa kijamii na kushambulia, wakati binamu yake Nour, ambaye alishiriki kwenye tukio hilo alishtakiwa kwa kosa la kushambulia.
Ahed Tamimi alijitetea kuwa alichukua hatua hiyo baada ya kuwaona wanajeshi wakimfyatulia risasi ya mpira kichwani binamu yake Mohammed mwenye miaka 15.
Wanajeshi wa Israel wamesema wamepeleka kikosi kwenye makazi ya Tamimi, ambapo vijana wa kipalestina wamekuwa wakirusha mawe kwa vikosi vinavyotuliza maandamano
Ahed Tamimi amesema alimkaripia mwanajeshi huyo alipompiga binamu yake kwa risasi za mipira
Vijana hao pia waliandamana dhidi ya tukio la kumsababishia Mohammed jeraha kichwani.
Kutokana na tukio hilo, Waziri wa Elimu wa Israel Naftali Bennett amesema Ahed na Nour Tamimi wanapaswa kufungwa maisha gerezani.
Raia wengi wa Israel wanasema kuwa Ahed Tamimi kwa muda mrefu amekuwa akitumiwa na familia yake, ambayo inashutumiwa kumtumia kuwaghadhabisha wanajeshi Israel.
Ahed Tamimi aliwahi kuonekana kwenye video nyingine akitishia kumpiga ngumi mwanajeshi mmoja
Ahed kwa mara ya kwanza alikuwa maarufu alipojitokeza hadharani akiwa na miaka 11, alionekana kwenye video nyingine akitishia kumpiga ngumi mwanajeshi mwingine.