Bunge la China lililoanza vikao vyake Jumatatu linatarajiwa kuidhinisha hatua za kuimarisha zaidi mamlaka ya Rais Xi Jinping ili kwenda sambamba na mabadiliko ya Katiba yaliyopendekezwa hivi karibuni.
Mabadiliko ya katiba yaliyopendekezwa kwenye mkutano wa mwaka wa bunge hilo ni pamoja na kujumuisha itikadi za kisiasa za Rais Xi Jinping kwenye sheria kuu ya China na kuondoa ukomo wa mihula ya Rais kuwa mamlakani.
Mapendekezo ya kuondoa ukomo wa mihula ya urais yanatarajiwa kuidhinishwa Machi 11 mwaka huu. Ikiwa yatapitishwa, Rais Xi ataweza kuendelea kuwa mamlakani bila ukomo baada ya kumalizika kwa mhula wa pili wa utawala wake mwaka 2023.
Mabadiliko makubwa ya nyadhifa katika nafasi za kiserikali pia ni miongoni mwa ajenda kuu za mkutano huo wa Bunge.
Mshirika muhimu wa Rais Xi Jinping, Wang Qishan amehudhuria mkutano huo wa bunge, sambamba na viongozi wengine.
Wang alimsaidia Rais Xi katika kampeni ya kukabiliana na rushwa nchini, lakini alistaafu kutoka kwenye Kamati Kuu ya Siasa ya Chama cha Kikomunisti mwaka jana, kwa mujibu wa umri wa kustaafu kwenye chama hicho.
Upo uwezekano mkubwa kwa Wang kupewa nafasi muhimu, huenda ya kuwa makamu wa rais na kuendelea kuwa na ushawishi katika diplomasia na kampeni ya kukabiliana na rushwa.