Bunge lazungumzia afya ya Spika Ndugai

 Spika wa Bunge, Job Ndugai anaendelea na matibabu nje ya nchi ikielezwa hali yake kuendelea vizuri.

Ndugai yupo kwenye matibabu nje ya nchi kwa muda sasa. Katika mkutano wa 11 wa Bunge, hakuonekana na ilielezwa kuwa yupo nje ya nchi kwa uchunguzi wa afya yake.

Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai amesema hali ya spika inaendelea vizuri na kwamba, anatarajia kurejea nchini wakati wowote.

"Ni kweli bado yuko nje ya nchi, lakini ifahamike kuwa afya yake inaendelea vizuri na wakati wowote atarejea nchini kuendelea na majukumu yake wala hakuna hofu kwa jambo hilo," amesema Kagaigai.

Hata hivyo, Kagaigai hakubainisha ni lini hasa kiongozi huyo atarejea na hakuzungumzia ugonjwa unaomsumbua wala nchi anayotibiwa, ingawa mara nyingi amekuwa akitibiwa nchini India.

Hii ni mara ya tatu kwa Ndugai kwenda nje kwa matibabu tangu aliposhika wadhifa wa Spika.

Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2016 ikiwa ni muda mfupi baada ya kuzinduliwa Bunge la 11.

Mara ya pili alikwenda mapema mwaka jana, lakini kipindi hicho hakukaa muda mrefu.

Afya ya Ndugai imekuwa ikiimarika na hata kuweza kukaa muda mrefu zaidi kwenye vikao anapokuwa Dodoma.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad