Chadema Yamjibu Msajili wa Vyama vya Siasa

Chadema Yamjibu Msajili wa Vyama vya Siasa
Wakati Chadema ikijibu barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kuhusu tuhuma za uvunjivu wa sheria ya vyama vya siasa na maadili ya vyama hivyo, huenda chama hicho kikakabiliwa na mambo matatu kama adhabu.

Chadema iliwasilisha majibu ya maelezo kuhusu tuhuma hizo jana katika ofisi ya msajili yakiwa ni ya pili baada ya yaliyowasilishwa awali kutomridhisha msajili.

Awali, Chadema ilitakiwa kutoa maelezo kwa kuvunja sheria kutokana na kufanya maandamano Februari 16 baada ya mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kinondoni uliofanyika Mwananyamala kwa Kopa jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuwasilisha majibu hayo wiki iliyopita, msajili alieleza kutoridhishwa na aliiandikia Chadema barua nyingine akitaka maelezo kuwa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe katika mkutamo huo wa kampeni alitoa lugha za uchochezi.

Katika barua zote mbili kwa Chadema, Jaji Mutungi amekitaka chama hicho kutoa maelezo ni kwa nini kisichukuliwe hatua za kisheria kwa kukiuka sheria ya vyama vya siasa na kanuni za maadili ya vyama hiyo.

Kwa mujibu wa kanuni za Oktoba Mosi, 2007 zilizosainiwa na Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa kifungu cha 6(1)(c)(d) zinaeleza wajibu wa msajili kwa vyama vya siasa.

Kifungu 6(1)(c) kinasema, “Kuzuia kitendo cha uvunjifu wa kanuni za maadili kisiendelee na kukitaka chama au kumtaka kiongozi wa chama kujirekebisha.”

Kifungu (d) kinasema, “Kutoa onyo la maandishi kwa chama au kiongozi wa chama husika.”

Kifungu (6)(2) kinaeleza, “Iwapo baada ya kutolewa onyo la kwanza kwa mujibu wa kanuni (1)(d), chama cha siasa kitaendelea au kiongozi ataendelea kukiuka maadili hayo, msajili atakemea hadharani ukiukwaji huo wa maadili.”

Hata hivyo, katika utekelezaji wa majukumu yake, msajili ana uwezo wa kuzuia ruzuku na hata kukifuta chama cha siasa.

Katika barua ya Chadema iliyosainiwa na Kaimu Katibu Mkuu, John Mnyika iliyowasilishwa jana kwenye ofisi ya msajili imeeleza masuala kadhaa yaliyowapata ikiwamo ya viongozi wake kutekwa, kuteswa, kushambuliwa na wengine kuuawa.

Chadema katika hoja ya kwanza inamweleza Jaji Mutungi kwamba katika barua yake, “Hujaeleza chanzo au sehemu ulipoyatoa maneno hayo na wala hujaeleza kifaa au chombo cha habari kilichotumika kunukuu maneno hayo iwe rahisi kwetu kutoa maelezo. Tuhuma zako hazina ushahidi wa aina yoyote ulioambatanishwa katika barua yako.”

Pili, Chadema inasema, Februari 27, Mbowe alihojiwa na Jeshi la Polisi katika Kituo Kikuu cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuhusu kauli aliyoinukuu Jaji Mutungi ambayo ni sehemu ya ushahidi mahakamani.

“Kwa kuwa bado shauri hilo la jinai halijamalizika na wakati huohuo ofisi yako inaendelea na uchunguzi wa kimaadili wa jambo hilohilo. Tunashauri usubiri jambo hilo limalizike kwa upande wa jinai kwa sababu ni ukiukwaji wa taratibu za kimahakama kwa mamlaka mbili tofauti kushughulikia jambo moja na lenye maudhui yanayofanana na kwa mtu yuleyule,” inasema Chadema.

Tatu, chama hicho kinasema hata kama maneno aliyonukuu yalitamkwa na Mbowe azingatie kuwa moja ya wajibu wa wanachama wa Chadema ambao umeainishwa katika Katiba ibara ya 5.3.5 ambayo yamenukuliwa:

“Kuwa tayari kupambana na namna yoyote ya uonevu, ukandamizaji, udhalilishaji na ubaguzi.”

Chadema imesema Mbowe kama mwanachama hakukosea kitu chochote katika maneno hayo kwa kuwa lugha hiyo ni wajibu wa mwanachama.

Hoja ya nne, Chadema inaeleza matukio kadhaa yaliyowafika viongozi wake tangu utawala wa awamu ya tano ulipoingia madarakani Novemba 5,2015 ikibainisha ni; kushambuliwa kwa risasi kwa mbunge Tundu Lissu, kupigwa kwa silaha za jadi kwa aliyekuwa mwenyekiti Mkoa wa Mwanza, Alphonce Mawazo Novemba 14, 2015 na kutekwa na kuumizwa kwa aliyekuwa mgombea udiwani wa Buhangaza wilayani Muleba mkoani Kagera, Nelson Makoti.

Pia, kutekwa, kuteswa hadi kuuawa kwa katibu wake wa Kata ya Hananasif, Daniel John, Februari 11 na kushambuliwa kwa mapanga na shoka hadi kuuawa diwani wa Namwawala wilayani Kilombero mkoani Morogoro, Godfrey Lwena.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad