Chadema Yawakana Viongozi Wake 12 Waliohamia CCM

Chadema Yawakana Viongozi Wake  12 Waliohamia CCM
Wimbi la wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuhama limeendelea kukikumba chama hicho kikuu cha upinzani nchini baada ya jana viongozi 12 wilayani hapa mkoani Tanga kuamua kujiunga CCM.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Handeni, Jadi Bamba alidai kuwa hao si viongozi bali ni wanachama wa kawaida na hawakuwa na nyadhifa zozote ndani ya chama.

Bamba alidai kuwa wanachama hao walishavuliwa nyadhifa zao na kupewa viongozi wengine wa mpito, hivyo hana taarifa za kuhama kwao na hafahamu lolote kuhusu suala hilo.

Takribani miezi sita sasa viongozi wa chama hicho, wakiwamo madiwani zaidi ya 25 wamehamia CCM, huku baadhi wakipitishwa na chama tawala kuwania nafasi hiyo na kuibuka na ushindi.

Akizungumza sababu za kuhamia CCM, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jimbo la Handeni Vijijini, Omari Wazafa alisema kazi ya wapinzani ilikuwa kuikosoa Serikali inaposhindwa kutekeleza mambo mbalimbali, lakini inatekeleza mengi.

Alisema awali, alikuwa kada wa CCM, lakini alipoona chama hicho tawala kinakiuka misingi ya kuanzishwa kwake, aliamua kuhamia Chadema.

Wazafa alisema wakati huo ndani ya CCM viongozi walishindwa kukemea maovu yaliyokuwa yakifanyika ndani ya Serikali na chama hicho, jambo alilodai ni tofauti na sasa.

“Serikali na chama sasa wana sauti, kwa kweli msimamo wa Rais, ndiyo ulionisukuma mimi na mwenzangu kurejea CCM,” alisema Wazafa.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Tanga, Omari Mwanga akimuwakilisha mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo, alisema changamoto zilizotolewa na wanachama hao watazifanyia kazi.

Alisema kuwa viongozi wote ambao wanaonekana kuwa kikwazo katika Serikali kwa kushindwa kuwaletea wananchi maendeleo hawana nafasi, hivyo anayejiona ameshindwa ajitoe mwenyewe.

Mkazi wa Komkonga, Suphiani Rashidi alisema kwamba viongozi hao wanaonekana kutokuwa na msimamo na vyama vyao ndiyo maana wanahama.

Pia alisema kwamba inawezekana wana masilahi binafsi katika kuhama kwao.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad