CHADEMA yazipelekea Barua Balozi za Marekani na Ujerumani Kuhusu Tuhuma za Musiba Kwamba zinaihujumu Tanzania
0
March 05, 2018
CHADEMA wazipeleka Video CD za Musiba Marekani na Ujerumani.
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimekwenda balozi za Marekani na Ujerumani kupeleka video zinazomuonyesha Cyprian Musiba akizituhumu nchi hizo kupanga mikakati ya kuhatarisha Usalama wa Taifa la Tanzania.
Akizungumza na JUPITA, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa chama hicho, Tumaini Makene amekiri chama chake kuandika barua yenye Kumbukumbu Nambari C/HQ/ADM/KS/24/02 iliyofika Ubalozi wa Marekani na yenye Kumbukumbu Nambari C/HQ/ADM/KS/24/01 iliyofikia Ubalozi wa Ujerumani,
Makene alisema barua ya Ujerumani ilielekezwa kwa Mkuu wa Kitengo cha Siasa na Uchumi, John Espinos huku ile ya Marekani ikielekezwa kwa Mkuu wa Kitengo cha Siasa na Uchumi wa nchi hiyo, Joerg Hererra.
“Tumeandika barua hizi tukizitaka nchi hizo zijibu tuhuma zilizoelekezwa kwao na Cyprian Musiba ambaye alisema Marekani kupitia FBI inaendesha mikakati ya kuhatarisha Usalama wa Tanzania.
“Lakini pia, Musiba alikihusisha chama tawala cha Ujerumani CDU kuwa kinashirikiana na Watanzania kula njama za kuhatarisha Usalama wa Taifa,” alisema Makene.
CHADEMA kupitia kwa Makene kimesema kiliguswa sana na tuhuma hizo na kikaona sio za kuzipuuza kwani ni tuhuma nzito na zisipofanyiwa kazi na kuachwa basi mipango hiyo inaweza kuliingiza taifa kwenye hatari kubwa huko mbeleni.
Makene anasema sambamba na barua hizo, pia chama chake kimeambatanisha CD za video zinazomuonyesha Musiba akiongea maneno hayo mbele ya vyombo vya habari Februari 25, 2018.
Chanzo: Media zote.
Tags