Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma imejipanga kupambana na kutokomeza mimba za utotoni katika Wilaya hiyo.
Akizungumza katika uzinduzi wa Kapeni ya Kutokomeza Mimba za Utotoni
katika Shule za Msingi na Sekondari katika Kata ya Haneti Wilayani
Chamwino, Diwani wa Kata ya Haneti Mhe. Peter Elia Chidawali amesema
kuwa Kata yake na Wilaya kwa ujumla wamejipanga katika kupambana na
vitendo vya ukatilia wa kijinsia yakiwemo matukio ya mimba na ndoa za
utotoni .
Mhe. Peter Elia Chidawali ameongeza kuwa hawatakubali kuona watoto
wao wanapoteza haki yao ya msingi ya kuendelezwa ya kupata Elimu kwa
kupata mimba au kuolewa wakiwa bado shuleni.
“Tutaendeleza Kampeni katika ngazi za familia kwa kuwaelimisha wazazi
na walezi kuhusu madhara ya mimba za utotoni ili tuokoe kizazi cha
kesho”alisema Mhe. Chidawali.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Watoto kutoka Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi Rose Minja
amesema kuwa suala la mimba za utotoni limezidi kuongeza siku hadi siku
hivyo basi Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
alizindua Kampeni ya Kutokomeza Mimba za utotoni kwa lengo la kuwezesha
utoaji wa elimu kwa wanafunzi, wazazi, walezi na jamii kwa ujumla
kushiriki mapambano dhidi tatizo hili.
“Wanafunzi, Walimu, Wazazi na walezi tuweke mikakati thabiti ya
kupambana na tatizo hili la mimba za utotoni” alisisitiza Bi. Rose.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya
ya Chamwino Bi. Shukuru Shanjala ameeleza kuwa Wilaya ya Chamwino
imejipanga katika kuzuia mimba za utotoni kwa kuhakikisha wanawafikia
wahusika katika ngazi za shule na familia na kutoa elimu kwa watoto wote
wa kike wanaowazunguka ili kuondokanana tatizo la mimba za utotoni
katika wilaya yao.
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto inaendelea na kampeni ya kuzuia mimba za utotoni chini katika
shule za Msingi na Sekondari ijulikanayo kama Mimi ni Msichana
Najitambua Elimu ndio Mpango Mzima sambamaba utekelezaji wa Mpango Kazi
wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na watoto katika
ngazi mbalimbali nchini ili kupunguza ukatili kwa asilimia 50 ifikapo
mwaka 2021/2022.