Soma Hizi Habari Zetu Kirahisi Kupitia Application ya Simu, Bonyeza HAPA
--------Upande wa utetezi umemlalamikia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kuchelewesha kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili aliyekuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi na wenzake.
Mbali ya Malinzi washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Joas Selestine na Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga.
Akiwasilisha malalamiko hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, Wakili wa utetezi Dominician Rwegoshora amedai kuwa DPP amekuwa akipitia jalada la kesi hiyo kwa muda mrefu.
Amedai kuwa kesi hiyo imechukua muda mrefu ambapo washtakiwa wapo rumande kwa takribani miezi 8 sasa tangu walipofikishwa kwa mara ya kwanza mwezi January 2017.
Naye Wakili Nehemiah Nkoko amedai kuwa hati ya mashtaka ipo wazi ambapo inaonesha risiti na kiasi cha fedha zinazodaiwa kuibiwa hivyo wanataka kuambiwa ukweli ni kitu gani kinachokwamisha upelelezi katika kesi hiyo kukamilika.
Hakimu Mashauri baada ya kusikiliza hoja hizo ameahirisha kesi hadi March 15, 2018 kwa ajili ya kutoa uamuzi.
Katika kesi hiyo, Malinzi na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 28 ya uhujumu uchumi ikiwamo kughushi na utakatishaji wa fedha dola za marekani 375,418.