Hali ya usafiri barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam leo asubuhi Machi 13, 2018 si shwari kutokana na uhaba wa mabasi ya abiria.
Vituo vingi vya daladala kutoka Mbagala hadi katikati ya Jiji vimekuwa na idadi kubwa ya abiria wakisubiri usafiri kuanzia saa 12 asubuhi.
Katika kituo cha Mbagala Rangi Tatu hali ilikuwa mbaya zaidi kutokana na kuwepo kwa abiria wengi wanaotoka pembezoni mwa viunga vya Mbagala.
"Nipo hapa tangu saa 12:30 na sijaliona gari la Makumbusho hadi muda huu. Magari ya maeneo mengine kama Posta na Kariakoo angalau yanakuja moja baada ya nusu saa, ila hizi ruti ndefu hakuna kitu," amesema Abdallah Lihende.
Naye Irene Gerars aliyekuwa kwenye kituo cha Mbagala Zakhiem amesema, "nimetoka kituo cha Rangi Tatu nimekuja huku angalau nipande gari la Buguruni nizunguke nalo nikaunganishe la Ubungo mbele ya safari, lakini tangu nifike hapa ni zaidi ya dakika 45 sijaliona gari la Buguruni hata moja.”
Mwandishi wa MCL Digital ameshuhudia vituo vya Kipati, Kizuiani, Misheni na Azizi Ally ambavyo ni nadra kuwa na abiria wengi wa kwenda na kurudi Mbagala vikiwa vimejaa abiria.