Hatimaye Wafuasi wa Mugabe Waunda chama cha Upinzani cha Kupambana na Mnangagwa

Hatimaye Wafuasi wa Mugabe Waunda chama cha Upinzani cha Kupambana na Mnangagwa

Jenerali mstaafu na mfuasi wa zamani wa Rais mstaafu Robert Mugabe, Ambrose Mutinhiri ameunda chama cha kisiasa ili kupambana na Rais Emmerson Mnangagwa katika uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.

Mugabe, mwenye umri wa miaka 94 alilazimishwa kustaafu Novemba iliyopita baada ya shinikizo la kijeshi.

Vyanzo karibu na kiongozi huyo wa zamani vinasema kuwa analalamikia namna utawala wake wa miaka 37 ulivyoondoshwa na anaunga mkono chama kipya cha New Patriotic Front (NFP).

Mutinhiri, mkongwe wa Zimbabwe aliyeshiriki vita vya kupigania uhuru miaka 1970 alijitoa kwenye chama cha Zanu-PF na kubwaga ubunge Ijumaa iliyopita, kisha alikutana na Mugabe Jumapili kumfahamisha maendeleo ya hivi karibuni, taarifa ya NPF ilisema.

Taarifa ya NPF imesema chama hicho kiliundwa na wafuasi wa Zanu-PF "waliokasirishwa na hatua isiyo ya kikatiba na udhalilishaji aliofanyiwa Mugabe kwa kuondolewa madarakani kama mhalifu ... na wahalifu wa kweli ambao wameharibu dhamana ya kidemokrasia nchini Zimbabwe".

Sera za Mugabe zimekuwa zikikosolewa na wengi kwa kusababisha Zimbabwe ishuke kutoka nchi yenye neema hadi kuwa isiyo na kitu, ukosefu wa ajira kuzidi asilimia 80, miundombinu ya umma iliyoharibika na uhaba mkubwa wa sarafu hali iliyozidisha mfumuko wa bei.

Chama hicho kipya cha upinzani kimesema kitafungua mashtaka kupinga uhalali wa serikali ya Mnangagwa katika Mahakama ya Katiba.

Hata hivyo, Novemba mwaka jana Mahakama Kuu ilitoa uamuzi kwamba hatua ya jeshi la Zimbabwe kuingilia kati ilikuwa halali kwa kuwa lilidhibiti jitihada za watu katika msafara wake kuchukua majukumu ya Mugabe na tayari nchi za Afrika na za Magharibi zimetambua urais wa Mnangagwa.

Gazeti la Herald linalomilikiwa na serikali ambalo huakisi mawazo ya Serikali lilisema kuwa Mutinhiri alikuwa shina lililokuwa nyuma ya siasa za Mugabe, mke wake Grace na kikundi cha G40 ndani ya Zanu-PF G40 kilichokuwa kinapinga kupanda kisiasa kwa Mnangagwa.

Mbali ya Mugabe na Grace, watu wengine waliopo nyuma ya chama hicho ni mawaziri waliopo uhamishoni Jonathan Moyo, Patrick Zhuwao na Saviour Kasukuwere.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad