Alitaja mambo hayo kuwa ni pamoja na hali ya uchumi, ajira kwa vijana, ughali wa matibabu na tangazo la elimu bure.
Mchungaji Njama ambaye pia ni mchungaji kiongozi wa Usharika wa Karanga mjini Moshi, alitaja mambo mengine kuwa ni hali ya kisiasa nchini na kundi kubwa la wastaafu kutolipwa mafao yao. Alitoa kauli hiyo jana wakati akiwasilisha taarifa yake katika mkutano mkuu wa 21 wa usharika huo wa Karanga, uliohudhuriwa pia na Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dk Martin Shao.
Mkutano huo mbali na kuhudhuriwa na mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Kati, Mchungaji Kennedy Kisanga na wachungaji wa sharika jirani, ulihudhuriwa pia na wawakilishi kutoka jumuiya 32.
Kauli ya Mchungaji Njama imekuja siku chache baada ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, (TEC) kuitaka Serikali ifufue mchakato wa uundwaji wa Katiba Mpya uliokwama.
Naibu Katibu Mkuu wa TEC, Padri Daniel Dulle alisema majadiliano yanahitajika ili kudumisha amani, heshima na kujenga taifa linaloheshimiana.
Hali ya uchumi
Akizungumzia hali ya uchumi nchini, Mchungaji Njama alisema awamu ya tano ilipoanza, watu walikuwa na mategemeo makubwa kwamba uchumi utaimarika lakini mambo yamekuwa tofauti.
“Umaskini unaendelea kuongezeka kwa nguvu. Tumeshuhudia biashara nyingi zikifungwa, wakulima wamekata tamaa, gharama za uzalishaji zimekuwa kubwa sana,” alisema Mchungaji Njama na kuongeza:
“Serikali haitoi ruzuku ila wakati wa kuuza mazao yao, wakulima hawajui wauze wapi na kwa bei gani. Wafugaji wanazalisha kwa gharama kubwa. Vyakula vya mifugo na dawa ni ghali.”
Hali ya kisiasa
Katika hotuba yake hiyo, Mchungaji Njama alisema kuna dalili za kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari na siasa.
“Inavyoelekea uhuru umeanza kuminywa. Ulianza kwenye siasa, ukaja kwenye vyombo vya habari... Kwa mfano takwimu za uchumi au chochote hata kama kina ukweli lakini utawala hautaki kusikia ukizungumzia hadharani au kwenye daladala ni kosa la jinai. Matukio ya miili kuokotwa yamezidi,matumizi ya risasi yameanza kuzoeleka kama kitu cha kawaida. Watu kupigwa risasi kwa walio wanasiasa na wasio wanasiasa yanafanya watu waishi kwa hofu.”
Baadhi ya matukio ya watu kupigwa risasi, ni pamoja na lile la Septemba mwaka jana, la Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu aliyeshambuliwa akiwa nje ya nyumba yake mjini Dodoma.
Kadhalika, tukio la hivi karibuni la mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini wakati wa maandamano.
“Hali hii ikiachwa, nchi itaingia kwenye umwagaji damu mkubwa,” alitahadharisha na kuungwa mkono na baadhi ya waumini.
Ukosefu ajira kwa vijana
Akizungumzia hali ya ajira nchini, Mchungaji Njama alisema miaka ya nyuma vijana walijua kwamba wakisoma watapata ajira, lakini leo imekuwa ni kinyume chake na karibu kila nyumba ina kilio.
“Karibu kila nyumba ina kijana aliyemaliza chuo kikuu au vyuo vya kati. Kundi la wasio na kazi limeongezeka maradufu na hii si dalili njema,” alisema.
Gharama za matibabu
Kwa upande wa matibabu, Mchungaji Njama alidai matibabu yamekuwa ghali akitolea mfano wa upasuaji wa kawaida kufikia Sh500,000 mbali na vipimo vya CT-Scan na MRI ambavyo ghamara yake pia kubwa.
“Watu wanashindwa kumudu gharama za matibabu. Bima za wasio na ajira za Serikali zinabagua matibabu na dawa. Wazee ambao wanapaswa kutibiwa bure imekuwa ni nadharia,” alidai.
Elimu bure
Mchungaji Njama alidai kuwa tangazo la elimu bure limeleta kushuka kwa elimu kuliko wakati wowote na kutolea mfano kuwa kati ya shule 100 zinazofanya vizuri, za Serikali ni chache.
“Ninashauri wajumbe wa mkutano mkuu tuwaelimishe wazazi wasicheze na maneno ya wanasiasa. Kuna msemo unaosema gharama ya ujinga ni kubwa kuliko gharama ya elimu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Askofu mstaafu Dk Shao, alilitaka kanisa hilo lisikae kimya na lichukue hatua ya kuzuia mafundisho potofu ndani ya kanisa, yanayotolewa na baadhi ya wachungaji.
Dk Shao alisema upungufu wa mafundisho ya kidini ni mkubwa na kuwataka wachungaji wa sharika za kanisa hilo, kutoruhusu kualika wahubiri wanaotoa mafundisho potofu kwa waumini.