HALI imechafuka na mambo si shwari hata kidogo! Sakata la majibizano
kati ya mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ au
‘Mondi’ na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana
Shonza, limezidi kuchukua sura mpya, Ijumaa linakuletea ukweli kamili wa
mtiririko wa majibizano hayo.
Mvutano huo ulianza kutimua vumbi mapema wiki hii na kukamata vilivyo
kwenye mitandao ya kijamii huku kukiwa na mpasuko mkubwa wa kimtazamo
kutoka kwa watu wa kada mbalimbali.
WAZIRI ALIKURUPUKA?
Akihojiwa katika Kipindi cha The Playlist cha Kituo cha Redio Times
FM cha jijini Dar, Diamond alimtuhumu Waziri Shonza kufungia nyimbo za
wasanii zikiwemo zake mbili za Halelluyah (aliowashirikisha Morgan
Heritage) na Wakawaka (aliomshirikisha Rick Ross) bila kuzingatia hasara
na usumbufu wanaoupata wakati wa kuziandaa kwa madai kuwa alikurupuka
tu kutoka nyumbani kwake na kuchukua hatua hiyo.
HAWA HAWAJAFURUKUTA
Wengine waliofungiwa nyimbo zao zilizo kwenye mabano ni Nay wa Mitego
(Pale Kati Patamu na Maku Makuz), Roma Mkatoliki (Kibamia), Man Fongo
(Hainaga Ushemeji), Nikki Mbishi (I am Sorry JK), Snura Mushi (Chura na
Nimevurugwa), Madee (Tema Mate Tuwachape), Jux (Uzuri Wako), Gigy Money
(Papa) na Barnaba (Nampaga) ambao wao hawakufurukuta mbele ya serikali.
Baada ya mahojiano hayo, Ijumaa lilizungumza na watu mbalimbali ili
kupata mitazamo yao kama Diamond alikuwa sahihi au la juu ya sakata
hilo.
JOYCE CHARLES WA KARIAKOO: “Diamond kumtishia waziri
ni kiburi cha fedha, unajua sasa hivi ana fedha hivyo anaona
ameshayapatia maisha bila kujua serikali ina mkono mrefu.”
YONA PLATNUMZ WA MBAGALA: “Kinachoonekana huyo waziri anaonea
wasanii maana hata wale wengine waliofungiwa wamekuwa wakilalamika
sema tu wao hawajapewa kipindi kwenye redio kama alivyopewa Diamond pale
Times FM.”
PAMELA DIVA WA SINZA:
“Kwa vyovyote kuna kitu nyuma ya pazia maana Diamond hajawahi kuwa
mwepesi kiasi hicho cha kurusha povu kwa viongozi wa serikali, sisi yetu
macho, lakini naamini kabisa kuna kitu kikubwa au kuna mkubwa anampa
kiburi Diamond.”
SIWEMA WA MAKUMBUSHO:
“Diamond hana lolote, ni mzee wa fursa, ameona kiki ya Zari kuuzia album imegoma sasa kaibuka na Waziri Shonza.”
RAYVANNY WA WCB:
“Mara nyingi thamani ya mtu na umuhimu wa mtu wengi wanaujua
akishaondoka… muziki ni kazi na ni ajira, ninamaanisha kuna familia
nyingi zinaishi kupitia muziki huuhuu.
“Katika wasanii wote Diamond amekuwa chachu ya kuongeza thamani ya muziki, kumbuka…ili mbegu iote, lazima ioze.”
QEEN DARLEEN WA WCB:
“Wakati baadhi ya watu nchini kwetu wanapambana kukushusha, nchi ya jirani inatamani kuwa na msanii kama wewe.”
FAIZA ALLY:
“Mungu akutunze baba.”
AUNT EZEKIEL:
“Woga wako ndiyo kufeli kwako Diamond…I’m so proud of you kiukweli
unajua unachokifanya, haijalishi anayetaka kukukatisha safari yako ni
nani na ana cheo gani! Ilimradi unajua haki yako, basi huweka woga
pembeni na kutetea haki yako…safi sana…”
WAZIRI SHONZA SASA
Kufuatia kuwepo kwa maoni hayo lukuki kwenye mitandao ya kijamii,
‘hotuba’ hiyo ya Diamond ilikuwa haivumiliki kwani pamoja na kusema kuwa
hataki kujibizana na msanii huyo, Waziri Shonza alimjibu:
“Siwezi kumjibu kwa sababu zipo taratibu za kufuata kama msanii hajatendewa haki.”
Katika maelezo yake, Waziri Shonza alisema kama kuna msanii anayeona
hakutendewa haki, milango iko wazi kuandika barua ya malalamiko.
Alisema kuwa, wasanii wanapaswa kuelewa kwamba hakuna aliye juu ya sheria hata kama ni msanii mkubwa kiasi gani.
DIAMOND TENA
Baada ya kusema hayo, Waziri Shonza alizua mjadala mpya kwani Diamond
alimjibu tena kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa hata yeye (naibu
waziri) alipaswa kuwaandikia barua wasanii kuhusu kuwafungia nyimbo zao.
MWAKYEMBE AMSHAMBULIA
Pamoja na Diamond kummwagia sifa kemkemu Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kuwa amekuwa msaada mkubwa kwa
wasanii kwa kuwashauri badala ya kuwafungia nyimbo zao, lakini naye
alimshambulia msanii huyo kwa kitendo chake cha kumdhalilisha Waziri
Shonza kwenye vyombo vya habari.
Juzi, Waziri Mwakyembe alionesha kukerwa na Diamond kutokana na
kumshambulia naibu wake na katika maelezo yake, Mwakyembe alisema
inaelekea sasa Diamond ameanza kusumbuliwa na umaarufu.
Kuhusu hoja ya vikao alivyodai mwanamuziki huyo kuwa huwa anakaa nao, Mwakyembe alisema:
“Kama ni vikao na wasanii, tumefanya vingi sana, lakini Diamond
hahudhurii vikao hivyo na si wajibu wa serikali kumfanyia kikao chake
mwenyewe, haijalishi ni maarufu kiasi gani.
“Hatuwezi kuwa na sheria kwa wasanii wengine na sheria maalum kwake,
nadhani hizi ni dalili za kuanza kulewa umaarufu kwani Diamond si
Kiongozi wa Shirikisho la Muziki wala msemaji wa Chama cha Muziki wa
Kizazi Kipya kuwasemea wenzake.”
USHAURI WA MWAKYEMBE
Waziri Mwakyembe alimshauri Diamond: “Si busara kwake kushindana na
serikali na kama ana ushauri, basi autoe kistaarabu utazingatiwa, lakini
si kwa kumshambulia naibu waziri kwa dharau na kejeli jinsi
alivyofanya. Sijafurahishwa hata kidogo.”
BASATA NAO
Kwa upande wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kupitia kwa katibu
wake mkuu, Godfrey Mngereza lilisema kuwa, Diamond amefanya makosa
kumjibu Waziri Shonza kwani huko ni sawa na kuitukana serikali.
“Maneno machafu anayoyatoa dhidi ya naibu waziri ni sawa na kuitusi
serikali, jambo ambalo hata ukienda katika sheria za kimtandao, anaweza
kujikuta anaingia matatizoni,” alisema Mngereza.
ALIANZIA KENYA
Kabla ya mambo hayo yote, Diamond alianza kumlalamikia Waziri Shonza
wiki iliyopita akiwa nchini Kenya kwenye uzinduzi wa albamu yake ya A
Boy From Tandale ambapo alikuwa akihojiwa na Kituo cha Redio cha Classic
FM cha nchini humo.
Alidai kuwa, viongozi hawafanyi utafiti kabla ya kutoa uamuzi.
“Naibu waziri amenizidi elimu, umri, mamlaka na vitu vingi, lakini
kwenye elimu ya sanaa nimemzidi hivyo alipaswa kunisikiliza kabla ya
kufungia nyimbo zangu.”
NINI KIFANYIKE?
Ni vizuri jambo hili likahitimishwa kwa kuwaweka chini wahusika wote
na kuwapa kanuni na taratibu za kiutendaji na sheria ya kuzifungia
nyimbo ili naibu waziri aachane na malumbano haya kwani Watanzania
hawayahitaji na badala yake wanataka maendeleo.
Huu Hapa Ukweli wa Sakata la Waziri Shonza na Daimond
2
March 24, 2018
Tags
Nafikiri si tatizo kubwa ila ni mambo ya management. Kama communication between wasanii na waziri ingekuwa ktk mfumo wa kiofisi yaani barua, wengine tusingeyajua yanayo endelea, ingekuwa ni kati ya waziri na wasanii. Barua naamini ingetoa fursa ya negotiations. Naamini bado wizara inahitaji reform. Sababu hili halisound km tatizo ila km aina tu ya udhaifu hasa ktk techniques za kumaintain stake holders
ReplyDeleteKama mzazi sifurahishwi na nyimbo zao za 'matusi', domo na asubiri hao watoto wake wakipata akili kisha awasikie wakiimba kile kipande katika wimbo wake wa 'ZILIPENDWA' pale Ray Vany alipoimba 'UFUNDI-KITANDANI-HUJATOMASA-UNACHANUA' kwenye video ndio aibu tupu.....linaonekana jitu kubwa linavua suruali....kama linataka kubaka vile....kwakweli HAPANA, sio wote tunapenda hizo nyimbo zisizo na tija kwa taifa wala vizazi vyetu....WAFUNGIWE TU........
ReplyDelete